
Utafiti
wa kisayansi katika tabaka la ozoni katika karne ya ishirini
ulithibitisha kumong’onyoka kwa tabaka hilo kutokana na kulundikana
angani kwa kemikali aina ya chloroflourocarbons (CFCs), halons, methyl
choroform, methyl bromide, carbon tertrachoridena nyinginezo.
Hayo
yalisemwa na Mkuu wa Chuo cha VETA– Chang’ombe Bi Vaileth Mfumbwa
wakati wa warsha ya mafunzo kwa Mafundi mchundo wanaoshughulikia
majokofu na viyoyozi ikiwa ni maadhimisho ya siku ya tabaka la ozoni
Duniani iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, iliyofanyika katika
Chuo cha VETA-Chang’ombe jijini Dar Es Salaam.
Aliongeza
kuwa Kemikali hizi hutumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya
kuzimia moto, ushafishaji chuma, utengenezaji wa magodoro, madawa na
manukato ya kupulizia, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na
mashamba ya maua na ufukizaji wa mazao katika maghala kabla ya
kusafirishwa nje ya nchi. Matumizi ya kemikali hizi yapo kwa wingi
katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea, kama Tanzania.
Akimkaribisha
Mgeni Rasmi, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Kemilembe Mutasa
alisema kuwa , Kitaifa maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya
Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yanafanyika jijini Dar es Salaam ambapo Ofisi
ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wakufunzi
wa Chuo cha Ufundi Dar es salaam wamepanga kutoa mafunzo kwa vitendo
kwa mafundi mchundo wanaohudumia majokofu na viyoyozi kuhusu njia bora
za kuhudumia vifaa hivyo; kutoa elimu jinsi ya kutumia vitambuzi vya
gesi; na kubadilisha tekinolojia zinazotumia kemikali haribifu kwa
tabaka la Ozoni kwa kemikali mbadala.
“Katika
maadhimisho haya, tunakumbushwa kuwa katika Mkutano wa 28 wa nchi
wanachama wa Mkataba wa Monteral uliofanyika nchini Rwanda mwaka 2016,
nchi wanachama zilikubaliana kupunguza uzalishaji na utumiaji wa
kemikali jamii ya Hydrofluorocarbons (HFCs) ambazo pia hujulikana kama
R-143a kwa jina la biashara na kukubaliana kuzuia ongezeko la joto la
dunia kwa nyuzi joto 0.5 (0.5 degrees Celsius)” alisema Bi. Mutasa
Warsha
hiyo ya mafunzo ya siku moja imekua chachu kwa Mafundi Mchundo
wanaoshughulikia majokofu na viyoyozi kwa kufundishwa njia mbalimbali za
kiutaalamu za kutumia wanapokua katika shughuli zao za kila siku.
Mafunzo hayo yalitolewa na Wakufunzi wa Chuo cha Ufundi-VETA Chang’ombe
jijini Dar Es Salaam.
Comments
Post a Comment