
Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Waziri
wa Madini Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuandaa haraka utaratibu
utakaowawezesha Wafanyabiashara wa Madini nchini kufanya shughuli zao
katika ngazi ya Kanda tofauti na ilivyo sasa ambapo taratibu zinawataka
kufanya shughuli hizo katika Mikoa zilipotolewa leseni zao.
Aliyasema
hayo Septemba 7, 2019 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao na
wizara uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi na Wataalam
wa wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Aidha,
Waziri Biteko alieleza kuwa, endapo wadau hao watafanya shughuli zao
kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa, serikali kupitia Wizara
ya Madini itaendelea kutanua wigo kuwawezesha kufanya biashara ya madini
katika maeneo mengi zaidi.
Waziri
Biteko alisisitiza kuhusu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli ya kutaka rasilimali madini kulinufaisha
taifa na watanzania na kueleza kuwa, ndoto hiyo ndiyo iliyopelekea
kufanyika kwa mageuzi mkubwa katika Sekta ya Madini.
Alikiri
kuwa, kabla ya mabadiliko hakukuwa na mfumo rasmi uliowaonesha
wachimbaji kujua sehemu sahihi ya kuuzia madini yao vivyo hivyo kwa
wanunuzi wa madini suala ambalo lilipelekea kuwepo vitendo vya
utoroshaji madini jambo ambalo lilionekana ni la kawaida.
Waziri
Biteko aliwataka wafanyabishara hao kuyatumia masoko yaliyoanzishwa
katika mikoa mbalimbali nchini na kusisitiza kuwa, serikali itaendelea
kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini na kueleza kuwa, waliobainika
kufanya vitendo hivyo wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na
hivyo kuwataka kuwa chanzo cha mabadiliko ili kuzuia vitendo vya
utoroshaji madini.
‘’
Tumekutana mpaka na wakemia wanaotengeneza madini feki. Kuna wengine
wataanza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunataka chumba cha madini
kiwe na hewa ya kutosha,’’ alisisitiza Biteko.
Akijibu
hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabishara wa Madini
ya Vito (TAMIDA) Sam Mollel, kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa
vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, Waziri Biteko aliwataka kuwa
na subira wakati serikali ikishughulikia suala hilo.
Aidha,
akijibu changamoto ya Masonara kusimamiwa na wizara nyingine,
Waziri Biteko aliwataka wafayabiashara hao kuwasilisha maoni kuhusu
suala hilo kama ilivyofanyika katika kuandaa Kanuni za Masoko na
kuongeza kwamba, ‘’ Tunataka kuwa wizara ambayo inatatua matatizo’’.
Naye,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisisitiza kuhusu suala la
kulipa kodi kama inavyowapasa na kuwataka kuyafahamu mabadiliko
yaliyofanywa katika sekta na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini, Dustan Kitandula, aliipongeza wizara kwa kazi ya kuwalea wadau
wa madini na kueleza kwamba, miaka ya nyuma mambo kwenye sekta hayakuwa
yakienda vizuri.
Aidha,
aliwapongeza wafanyabiashara wa madini na kueleza kuwa, hivi sasa
wameanza kubadilika huku tabia ya kufanya biashara ya madini kiholela
ikianza kutoweka.
‘’ Sisi Kamati tunapoona mambo yanakwenda vizuri mnaturahisishia kazi yetu’’, alisisitiza Mwenyekiti wa Kamati.
Kikao
hicho kimefanyika ikiwa ni jitihada za wizara za kuendelea kutoa elimu
kwa wadau wa madini ikiwemo kusikiliza na kutatua changamoto kwenye
sekta ili kuwezesha biashara ya madini kufanyika katika mazingira
mazuri yanayoleta tija kwa pande zote.
Aidha,
sambamba na mkutano huo, imefanyika Semina kwa Wabunge wa Kamati ya
Kudumu ya Nishati na Madini kubwa ikiwa ni serikali kueleza nia yake ya
kukifanya Chuo Cha Madini Dodoma kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Akifunga
semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula alitaka mchakato wa
wa kukilea Chuo hicho kutochukua muda mrefu na alikitaka kijisimamie
chenyewe ndani ya muda mfupi baada ya kulelewa na kutoa elimu bora.
Pia, alitaka kozi ya Mafundi Mchundo kuwekewa msingi mzuri.
Pamoja
na hayo, Mwenyekiti wa Kamati aliitaka wizara kukiongezea nguvu Kituo
Cha Jimolojia Tanzania (TGC) ikiwemo bajeti ya kutosha kukiwezesha
kuboresha miundombinu yake
Comments
Post a Comment