Tanzania Yachaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Nchi Zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA)


Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa nchi za Afirika zinazozalisha Almasi katika Mkutano wa Mawaziri wa nchi hizo unaofanyika Widhoek nchini Namibia kwa siku mbili kuanzia jana tarehe 8 Julai 2019.

Mwenyekiti mpya wa nchi za Afrika wazalishaji wa Almasi ni Namibia ambaye amepokea kijiti kutoka kwa Guinea.

Kwa hatua hiyo Tanzania itakuwa Makamu Mwenyekiti kuanzia sasa hadi mwezi Julai mwaka 2020 ambapo atakuwa Mwenyekiti kamili kulingana na kanuni za ADPA.

Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameiwakilisha Tanzania katika mkutano huo maalumu kwa kuitikia mwaliko wa Waziri wa Nishati na Madini wa Namibia kushiriki katika Mkutano huo wa 6 wa Mawaziri kutoka nchi za Afirika zinazozalisha madini ya Almasi.

Akizungumza na mtandao wa Wazohuru Mhe Biteko amesema kuwa mapokeo ya nafasi ya Tanzania kuwa makamu mwenyekiti katika Mkutano huo utafanyika tarehe 8 na 9 Julai, 2019 katika jiji la Windhoek nchini Namibia ni sehemu ya heshima ya Tanzania katika uwajibikaji hususani katika utendaji makini wa usimamizi wa rasilimali Madini.

Alisema kuwa Tanzania kushiriki Mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni miongoni mwa nchi zinazozalisha Almasi barani Afrika.

Aidha, katika mkutano huo Waziri Biteko amepata fursa ya kujifunza zaidi  kuhusiana na usimamizi wa sekta ya madini hususani madini ya Almasi kutoka nchi mbalimbali zinazoshiriki.

Miongoni mwa madhumuni ya mkutano wa nchi zinazozalisha almasi (ADPA) ni pamoja na Kuwa na umoja ambao utasaidia nchi za Africa ziweze kunufaika na Madini ya Almasi yanayozalishwa katika nchi hizo na Kusaidia wachimbaji wadogo kupata bei nzuri ya Madini wanayozalisha.

Kadhalika, Kubadilishana uzoefu katika kuendesha sekta hiyo kutoka nchi moja na nyingine, na Kuwa na Sera zinazoenda kati ya nchi hizo kuhusiana na masuala ya sekta ya Almasi kama vile utafiti  , uchimbaji, uongezaji thamani n.k

Madhumuni ya umoja huo ulianzishwa tarehe 4 Novemba, 2006 kwa azimio lijulikanalo kama Declaration of Luanda ambapo Tanzania atakuwa mwenyeji wa kikao kijacho kitakachofanyika mwezi Julai, 2020.

Mhe Biteko amesema kuwa nchini Tanzania Leseni zilizotolewa kwenye almasi ni Leseni kubwa za uchimbaji (SML) 2, leseni ndogo za uchimbaji (PML) 93, leseni ndogo za biashara (Brokers) 15 na leseni kubwa za biashara (Dealers) 16.

Aliongeza kuwa Sekta ya almasi imeajiri takribani watu 2,600 wanaojishughulisha moja kwa moja na shughuli za biashara na uchimbaji.

Comments