1.Katika
kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali
inaendelea, pamoja na mambo mengine, kuimarisha mazingira ya uwekezaji
na ufanyaji biashara katika sekta mbali mbali hapa nchini, ikiwemo sekta
ya usafirishaji. Sekta hii ni miongoni mwa Sekta zenye mchango mkubwa
katika kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, sekta hii
imekuwa ikichangia pia kuzalisha ajira kwa vijana wetu katika nafasi
mbali mbali kama vile Madereva, Mafundi na kada nyingine nyingi.
2.Pamoja
na mchango mkubwa unaotolewa na sekta hii, zipo changamoto kadhaa
ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na Serikali kwa kushirikiana na wadau.
Kwa upande wa utekelezaji wa Sheria za Kazi, changamoto zimeendelea
kujitokeza katika masuala ya Mikataba ya Ajira, Malipo ya Mishahara na
Posho mbali mbali, ambapo imebainika yapo Makampuni machache yanayolenga
kuchafua kazi nzuri inayofanywa na sekta hii, ambapo makampuni hayo
machache yamekuwa yakifanya udanganyifu kwenye Mikataba ya Ajira za
Madereva wao pindi yanapofanya maombi ya Leseni za Usafirishaji.
3.Aidha,
katika jitihada za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi; Kitengo cha Usalama Barabarani na LATRA inatarajia kufanya Zoezi
Maalum la Ukaguzi kwa lengo la kukagua Mikataba hiyo na kuangalia
utekelezaji wa Sheria kwa ujumla.
4.Zoezi
hili linatarajiwa kufanyika kwa namna mbili tofauti ambapo; (i) Maafisa
Kazi waliopo katika Ofisi za Kazi watapita katika Kampuni zote za
Usafirishaji na (ii) Timu maalum ya Maafisa Kazi wa kushirikiana na
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva, LATRA na Jeshi la Polisi;
Kitengo cha Usalama Barabarani watafanya Ukaguzi wa Mikataba kwenye
Vituo Vikuu vya Ukaguzi kama vile Kituo cha Mabasi Ubungo, Kituo cha
Kuegesha Malori cha Misugusugu na vituo vingine vinavyofanana na hivyo
hapa nchini.
5.Aidha,
sambamba na ukaguzi huo, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na
Vyama vya Waajiri watapatiwa elimu kuhusu haki na wajibu wao katika
kutekeleza Sheria za Kazi.
Hivyo,
ninapenda kuwaarifu Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji, Wafanyakazi
Madereva na Umma kwa ujumla kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu inatarajia kuanza rasmi Zoezi la Ukaguzi wa
Mikataba ya Ajira ya Madereva na Utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa
ujumla ifikapo tarehe 15 Julai, 2019.
6.Ili
kulifanya zoezi hili kuwa lenye ufanisi, ni vema Wamiliki wa Vyombo vya
Usafirishaji kuhakikisha kuwa Mikataba ya Madereva wenu inakuwepo
katika maeneo yenu ya kazi, na kwa upande wa Madereva, kuhakikisha
mnakuwa na nakala za Mikataba yenu mnapokuwa katika kazi zenu ili iwe
rahisi kwa Wakaguzi kuiona.
7.Aidha,
ninapenda kuwaarifu kuwa Zoezi la Ukaguzi wa Mikataba ya ajira na
Utekelezaji wa Sheria kwa ujumla litakuwa endelevu na litaendelea pia
katika Sekta nyingine hapa nchini.
8. Mwisho, ninapenda kutoa wito kwa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva pamoja na Madereva
wote nchini kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wakaguzi wakati wote wa
utekelezaji wa zoezi hili ili kutoathiri utoaji wa huduma kwa wananchi
kwa namna yoyote ile.
IMETOLEWA NA
KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU
3/7/2019
Comments
Post a Comment