Waziri wa Madini wa Tanzania aunguruma kwa dakika tano Paris

Waziri wa madini Doto Biteko
 *Paris* Serikali imeahidi kuendelea kutekeleza sera ya uwazi na
uwajibikaji katika ulinzi na matumizi ya rasilimali ya Taifa kwa lengo
la kuwanufaisha wananchi na Taifa.

Akihutubia mkutano wa nne wa Kimataifa wa tathmini ya mkakati wa Uwazi
na Uwajibikaji katika Ulinzi wa Rasilimali za nchi (EITI) jijini Paris,
Ufaransa jana Juni 18, 2019, Waziri wa Madini, Dotto Biteko ametaja moja
ya mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni urasilimishaji wa shughuli za
wachimbaji wadogo wa madini.

“Mpango huo unaohusisha Serikali, wachimbaji wadogo na wadau wengine wa
sekta ya madini, umefanikishwa na uwepo wa sheria na uwazi na
uwajibikaji iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
mwaka 2015. Mchango wa sekta ya madini kwenye pato na uchumi wa Taifa
umeanza kuongezeka,” amesema Biteko.

Katika hotuba yake ya dakika tano kwa wajumbe, Waziri Biteko anayeongoza
ujumbe wa Tanzania katika mkutao huo ameahidi kuwa Serikali itaendelea
kutekeleza makubaliano ya Kimataifa kuhusu uwazi na uwajibikaji katika
sekta na nyanja zote za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kamati ya EITI Tanzania (TEITI), Ludovick Uttoh emetaja
moja ya faida ya uwazi na uwajibikaji katika ulinzi na matumizi ya
rasilimali za Taifa ni kutoa fursa na haki kwa wananchi kupata taarifa
muhimu za miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Mjumbe wa EITI Tanzania, Blandina Sembu ametaja uzingatiaji wa masuala
ya jinsia, hasa umiliki na matumizi ya ardhi kwa wanawake kuwa miongoni
mwa faida na mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera ya uwazi na
uwajibikaji katika usimamizi na matumizi ya rasilimali.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa EITI, Fredrik Reinfeldt amesisitiza
umuhimu wa uwazi na wajibikaji katika usimamizi na matumizi ya
rasilimali za Taifa kutokana na mafanikio yaliyopatikana tangu mikakati
hiyo ilipoanza kutekelezwa.

Mratibu wa Taasisi ya Haki Rasilimali ya Tanzania, Recho Chagonja
amesema Mataifa ya Afrika ambao ni wadau wakubwa wa utekelezaji wa
mpango huo yanatakiwa kufanyia mabadiliko baadhi ya sera na sheria zake
ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye rasilimali za Taifa.

Comments