
Umoja
wa Afrika AU umechukua uamuzi wa kusimamisha uanachama wa Sudan katika
jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Afrika mpaka pale Baraza la Kijeshi
litakapokabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Umoja huo pia umesema unajadili suala la kuwawekea vikwazo maafisa wa
jeshi la Sudan waliohusika na mashambulizi dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Taarifa
hiyo imetolewa katika kikao cha dharura cha Baraza la Amani na Usalama
la Umoja wa Afrika kinachokutana mjini Addis Ababa huko Ethiopia kwa
ajili ya kutathmini hali ya mambo nchini Sudan.
Katika
kikao hicho pia Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limelaani
tena mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Sudan na kupinga mabadiliko ya
aina yoyote yasiyokuwa ya kikatiba.
Msimamo huo wa Umoja wa Afrika umechukuliwa huku Baraza la Kijeshi
lililotwaa madaraka nchini Sudan likiendelea kukabiliwa na upinzani
mkali wa wananchi na vyama na makundi ya upinzani yanayosisitiza kuwa
yataendelea kufanya maandamano na migomo ya kijamii hadi pale wanajeshi
watakapokabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.
Comments
Post a Comment