WAZIRI MPINA ATOA ONYO KWA WATUMISHI WANAOKAMATA MIFUGO NA KUISHIKILIA HADI KUFA IKIWA MIKONONI MWAO




Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina  amesema serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria  watu wanaofanya ukatili kwa wanyama ambapo amesema ifikapo tarehe 1.Julai ,2019  watendaji wanaoshikilia mifugo hadi kufa ikiwa mikononi mwao  watashughulikiwa. 



Mhe.Mpina amesema hayo leo Mei 22,2019 Bungeni jijini Dodoma  ambapo amesema  mifugo ni rasilimali za nchi kama rasilimali nyingine na wizara yake haitavumilia kuona mtendaji wa Serikali akishikilia mifugo mpaka ina kufa kwa kigezo cha kufuata sheria kwani hata mifugo nayo ina sheria zake. 



Awali ,Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega wakati akijibu swali la mbunge wa Wa Morogoro Kusini  Prosper Mbena aliyehoji  juu ya ukatili wa wanyama kushamiri nchini ,chama cha kuzuia ukatili wa wanyama Tanzania ,TSPCA  kina shirikiana kwa kiasi gani na Serikali ili kuzuia ukatili ,Mhe.Ulega amezitaja sheria za wanyama pindi wanapokamatwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa malisho,maji na chanjo. 



Kuhusu uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata na kusindika nyama katika maeneo yaliyo karibu na wafugaji ili kupunguza ukatili wa wanyama pindi wanaporundikwa kwenye magari wakati wanaposafirishwa Kwenda Dar Es Salaam  kwa ajili ya kuchinjwa,Mbunge wa Msalala  Ezekiel Maige  amehoji lini serikali itaanzisha viwanda  katika maeneo mbalimbali ya wafugaji nchini ikiwa ni pamoja na Shinyanga. 



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mchakato wa kufufua viwanda vya kuchakata na kusindika  nyama nchini upo palepale  na kinachotakiwa ni kupata mwekezaji aliyejipanga vizuri.
Hata hivyo,Serikali inashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali  kama TSPCA  katika kudhibiti vitendo vya kikatili kwa wanyama  kwa kuzingatia sera ya mifugo  ya mwaka 2006  na sheria ya Ustawi wa wanyama ya mwaka 2008 kwa kuelimisha jamii. 



Mwaka 2018 jumla  ya Makosa  3,542 kwa kosa la ukatili wa wanyama yaliripotiwa  ambapo ni  ng’ombe  847 ,mbuzi na kondoo 1,578,nguruwe 88,kuku 539 na punda 490.

Comments