
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa
nchini, Mhe. Pekka Hukka na kumshukuru kwa jitihada za nchi hiyo
kuisadia Tanzania kuondokana na umaskini.
“Tunaishukuru Serikali ya Finland kwa misaada ambayo imeendelea kuitoa
kama njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuondoa
umaskini pamoja na kuongeza makusanyo ya mapato ili kukuza uchumi wa
nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo (Alhamisi, Mei 23, 2019) alipokutana na Balozi
huyo anayemaliza muda wake wa kazi hapa nchini, ofisini kwake bungeni
jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amemweleza balozi huyo kwamba Tanzania bado ina fursa za
uwekezaji na kwamba Serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki na
bora kwa uwekezaji. “Sekta ambazo makampuni ya Finland yanaweza kuwekeza
hapa nchini ni pamoja na TEHAMA, nishati, usafiri, uchakataji wa mazao
ya kilimo na misitu,” amesema.
Waziri Mkuu alimtakia heri Balozi Hukka ambaye anatarajiwa kuondoka
nchini mwishoni mwa mwezi huu kwenda Tunisia ambako ndiko kutakuwa na
kituo chake kipya cha kazi.
Kwa upande wake, Balozi Hukka alisema ataondoka Tanzania akiwa na
kumbukumbu nzuri ambazo atazienzi na anataraji kukutana na Watanzania
wengine ili aendelee kukuza mahusiano yaliyokuwepo.
Alisema Serikali za Tanzania na Finland zilisaini mkataba wa programu
iitwayo Forestry and Value Chain Programme (FORVAC) ambao unalenga
kuongeza faida za kiuchumi na kijamii kwa kupitia sekta ya misitu pamoja
na kupunguza ukataji wa miti. “Malengo hayo yatafikiwa kwa kukuza
mnyororo wa thamani kwenye sekta ya misitu pamoja na kuimarisha mifumo
ya ufuatiliaji, sheria na sera katika sekta ya misitu,” alisema.
Finland inasaidia sekta ya misitu nchini Tanzania kupitia Programu ya
Private Forestry Programme (PFP) ambayo ililenga kuongeza mapato kwa
wakazi wa vijijini katika Halmashauri 10 za Njombe TC, Njombe DC,
Makete, Ludewa, Kilombero, Mufindi, Kilolo, Madaba, Mbinga na Nyasa) kwa
kusaidia upandaji wa miti na kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Programu hiyo imesaidia kujenga uwezo kwa wahusika wote katika mnyororo
wa thamani wa biashara ya mazao ya misitu. Awamu ya kwanza ya programu
hiyo imesaidia kuongeza kipato cha familia zaidi ya 9,000 kwenye wilaya
hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekutana na Balozi wa Uswisi hapa
nchini, Mhe. Florence Mattli ambaye pia alienda kumuaga ofisini kwake
bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu alimweleza balozi huyo dhamira ya Serikali ya Tanzania ya
kudumisha ushirikiano na Uswisi na kusisitiza kwamba iko tayari kufanya
kazi na Balozi mpya wa Uswisi atakayekuja kwa manufaa ya pande zote
mbili.
“Ni muhimu sana ushirikiano wa Tanzania na Uswisi ukadumishwa kwa
kuzingatia pia masuala ya biashara na uwekezaji hususan kwenye sekta za
afya, kilimo, elimu na teknolojia,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Uswisi kwa misaada ambayo
imeendelea kutolewa na nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada za
Serikali ya Tanzania za kuondoa umaskini hususan kwenye miradi ya afya,
kilimo na uwekezaji katika elimu na biashara kwa ajili ya kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Balozi Mattli alisema Serikali ya Uswisi imekuwa
ikiunga mkono na kusaidia jitihada za kukuza uwazi na uwajibikaji kwa
watendaji wa Serikali na wale wasiokuwa wa Serikali kuzingatia mazingira
ya kitaasisi na kijamii yanayopiga vita masuala ya rushwa.
“Msaada huo wa kupambana na rushwa umechangia kuimarisha ufanisi wa
uendeshaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
kukuza uelewa wa kijamii kuhusu masuala ya rushwa,” alisema.
Alisema mwaka 2018, Serikali ya Uswisi ilitoa dola za Marekani milioni
24 kusaidia Mpango wa Ukuzaji Ujuzi kwa Ajira Tanzania, ambao ulianza
kutekelezwa Agosti Mosi, 2018 kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia.
“Mpango huo unalenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa vitendo na
kuimarisha mafunzo ya ufundi nchini. Hivyo, mpango huo umechangia
kuboresha matarajio ya vijana kwa kuwapatia ujuzi katika kazi na ubunifu
unaochangia kuondokana na suala la ukosefu wa ajira,” alisema.
Alisema Serikali ya Uswisi inasaidia maendeleo ya vijana kupitia Mpango
wa Ajira ya Vijana (OYE) ambao unalenga kuimarisha maisha ya vijana wa
kiume na wa kike kwa kuwafundisha fursa za ajira katika sekta za
biashara, kilimo, nishati mbadala, usafi wa mazingira na kuboresha
ujuzi.
Comments
Post a Comment