Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameondoka nchini kwenda Afrika ya
Kusini ambapo kesho atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa
nchi hiyo, Cyril Ramaphosa.
Katika safari hiyo Rais Magufuli
ameongozana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Philip Mangula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi.
Wakizungumza kabla ya kuondoka, Rais
Mstaafu Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM Ndg. Mangula wamesema
Tanzania na Afrika ya Kusini zina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na
kwamba Serikali na chama zina kila sababu ya kudumisha uhusiano na
ushirikiano huo.
Viongozi hao wameondoka katika uwanja
wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa
kutumia ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema baada ya
kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Afrika ya Kusini,
Rais Magufuli atafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia ambako pia
atazindua mtaa uliopewa jina la Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius
Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa katika ukombozi
wa Taifa hilo.
Comments
Post a Comment