Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewatangazia kiama askari wa
Kikosi cha Usalama Barabarani nchini wanaowabambikia madereva makosa ya
picha za mwendokasi (Speed rader) zisizo na uhalisia kwa nia ya
kujipatia mapato wakibainika watawajibika kuzilipa wao wenyewe faini
hizo na kuondolewa katika kitengo hicho.
Alitoa
agizo hilo mjini Morogoro wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu
maafikiano kati ya vyama vya watoa huduma za usafirishaji nchini kuhusu
kusitisha kusudio la madereva wa mabasi ya abiria kufanya mgomo
wakishinikiza kutimiziwa madai yao mbalimbali ikiwamo ya mikataba ya
kazi.
Alisema
maamuzi hayo yametokana na makubaliano ya pamoja baina viongozi wa
vyama hivyo vya usafirishaji pamoja na wizara mtambuka za serikali kwa
nia ya kutatua changamoto walizowasilisha katika kikao hicho kuhusu
kubambikiwa makosa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Waziri
Lugola, alisema moja ya makosa yanayolalamikiwa na madereva hao ni
pamoja tochi zinazopiga picha mabasi na kurushwa kwenye simu za maaskari
zinakosa uhalisia wa tukio ikiwamo kutoonekana kwa namba za usajili
pamoja na vibao vya kuzuia makatazo mbalimbali na kusababisha utata na
mivutano yenye nia ya kujenga mazingira ya rushwa.
Alisema
kuanzia sasa askari hao wanapaswa kupiga picha katazo mbalimbali za
barabara mbele ya gari ikionyesha mwonekano usio na mashaka, namba ya
usajili pamoja na eneo la alama iliyokiukwa na dereva ili kuwapo na
ushahidi halali vinginevyo dereva huyo asichukuliwe hatua yoyote.
“Dereva
anapokuwa na mashaka na picha iliyopigwa dhidi ya gari lake kama
haionyeshi usajili wa namba za gari na eneo la kibao cha zuio asikubali
kuadhibiwa na badala yake amweleze huyo askari azitume picha hizo kwa
msimamizi wa kikosi cha usalama barabarani na aende huko,” alifafanua
Waziri Lugola.
Pia
alisema tabia ya baadhi ya askari kukamata mabasi yenye abiria na
kuyafikisha kituo cha polisi kwa nia ya kumuadhibu dereva aliyetenda
makosa, jambo hilo liachwe mara moja na badala yake dereva aliyetenda
kosa anapaswa kukamatwa katika kituo cha mwisho cha safari yake.
“Sheria
ya Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), inaeleza
wazi kila basi linalofanya safari za masafa marefu lazima liwe na
madereva wawili, hivyo ukimkamata dereva na kumweka ndani tayari unaenda
kinyume na sheria za Sumatra na kulifanya basi kushindwa kuendelea na
safari yake,” alisema.
Aidha,
aliliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani
kuendelea kuwanyang’anya leseni madereva wanaofanya makosa ya kujirudia
pamoja na kukamata magari yanayofanya shughuli za usafirishaji bila kuwa
na leseni kwa kushirikiana na Sumatra.
Comments
Post a Comment