
Katika
kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018/19, zaidi ya shilingi Bilioni 93.8
zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu ya shule 588 ambapo shule
303 ni za msingi na sekondari 285.
Hayo
yameelezwa leo, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia, William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Bumbwini, Muhammed Amour Muhammed juu ya juhudi zipi za makusudi ambazo
Serikali inakusudia kuchukua ili kupandisha hali ya ufaulu wa wanafunzi
wa kidato cha Nne.
"Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi
mbalimbali za Elimu. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia kwa kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa
miundombinu katika shule mbalimbali za Serikali nchini," amesema Ole
Nasha.
Ole
Nasha amesema kuwa uboreshaji wa miundombinu uliofanyika katika shule
hizo 588 umehusisha madarasa 1,190, mabweni 222, vyoo 2,141, mabwalo 76
na nyumba 99.
Ameongeza
kuwa, Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia
vikiwemo, vifaa vya maabara katika shule, na vifaa vya kielimu kwa
ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha
Naibu Waziri Ole Nasha ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2017
hadi Aprili 2019 Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,884 ili
kukabiliana na uhaba wa walimu nchini.
Vile
vile Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule
kwa kununua na kusambaza magari 45 ya Uthibiti Ubora wa Shule na
Pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu kata na kuongeza kuwa katika
Mwaka wa Fedha 2019/2020 Serikali inatarajia kujenga ofisi 100 za
wathibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi.
Comments
Post a Comment