RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haina mpango wa kuongeza
maeneo ya utawala ikiwemo kuanzisha mikoa mipya na badala yake
imejipanga kuimarisha huduma na mahitaji ya miundombinu iliyopo ili
kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya
Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru yenye urefu wa kilometa 193 Jana (Ijumaa April 5, 2019), Rais Magufuli alisema Serikali imekusudia
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ujenzi wa
miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu n.k katika maeneo waliopo.
Aliongeza kuwa katika awamu yake yake ya Uongozi, suala la kuongeza
maeneo ya utawala halipo na badala yake kuwataka Viongozi wa maeneo hayo
wajipange katika kuwaletea maendeleo wananchi badala ya fedha zilizopo
kwenda katika kujenga ofisi mpya za Wakuu wa Mikoa mipya na kuwalipa
mishahara viongozi hao.
“Tumepanga kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu, tumechelewa
kuleta Maendeleo hususani kwa wananchi wetu wa mikoa ya kusini, Serikali
ninayoiongoza haina mpango wa kuanzisha mikoa mipya , badala yake pesa
hizo tutazielekeza katika ununuzi wa madawa na kuboresha miundombinu ya
barabara, elimu na nishati’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema bado yapo baadhi ya maeneo mengi nchini
yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara za lami, hivyo
Serikali haitoweza kuleta Maendeleo katika sehemu moja kwa kuwa fedha
hizo hazipo kwa kuwa ina na mahitaji makubwa katika kuboresha huduma
mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha
kuwa huduma muhimu na za msingi kwa Maendeleo ya wananchi zinapewa
kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati, kwa kuwa
kukamilika kwake kutasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto
ambavyo katika miaka ya nyuma vimekuwa vikisababisha vifo vya makundi
hayo ya kijamii.
Akizumgumzia kuhusu Sekta ya Maji, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa
Maji, Prof. Makame Mbarawa kuwasimamia wakandarasi wa miradi ya maji
nchini, kwani Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha cha fedha
katika miradi ya Maendeleo pasipo na kupata matokeo yaliyotarajiwa, na
hivyo kuisababishia hasara Serikali.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Fedha na Mipango, miradi mingi ya
maji imekuwa ikitumia fedha nyingi pasipo na kupata matokeo yoyote na
wataalamu wetu hasa wakandarasi wamekuwa wazito kutoa tafsiri za
nadharia za utaalamu na kuzileta katika nadharia halisi, na mataifa ya
nje yanashangwa tunaposhindwa kuvitumia vyanzo tulivyonazo ili kuweza
kuzalisha maji ya kutosha’ alisema Rais Magufuli.
Awali akizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kujengwa kwa barabara
hiyo kutaimarisha mawasiliano katika ukanda wa kusini unaojumuisha
Mtwara, Mingoyo, Masasi, Mangaka, Tunduru hadi Mbamba Bay na hivyo
kuzidi kufungua fursa za kiuchumi nanchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Alisema hadi kukamilika kwake barabara hiyo imegharimu kiasi cha Tsh
Bilioni 173, ambapo Shirika la Misaada la Japan limetoa asilima 23.24,
Benki ya Maendeleo ya Afrika asilimia63.32 na Serikali ya Tanzania
asilimia 13.35 ikiwemo kodi na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili
kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto alisema Serikali ya
Japan imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya
maendeleo ikiwemo barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru na
itaendelea kusaidia miradi mingine ili kuhakikisha kuwa malengo ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuondoa umaskini kwa wananchi wake
yanafikiwa.
Comments
Post a Comment