Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
amemuapisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango
atakayeshughulikia sera Adolf Hyasinth Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi,
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu,
Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa Wizara
ya Fedha na Mipango.
Akizungumza baada ya
kuwaapisha, Rais Magufuli ameitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango
kupanua uwigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo
vipya vya mapato, pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi
zaidi kulipa kodi ili kuongeza makusanyo ya kodi.
Rais Magufuli
ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa TRA ambayo mpaka sasa
inakusanyaji kodi kwa walipa kodi Milioni 2 na Laki 7 tu kati ya
Watanzania wote zaidi ya Milioni 55, na amesema kwa mtindo huo TRA
itakuwa inazidi kuwakamua walipa kodi wachache wakati ingeweza kupanua
uwigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na
vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi.
“Ukienda
mipakani wafanyabiashara wanafungua maduka upande nchi za wenzetu na
sio upande wa Tanzania, na sababu ni kwamba wakifungua upande wa
Tanzania wanasumbuliwa na TRA, wekeni viwango vya kodi vinavyolipika ili
watu wengi waweze kulipa kodi badala ya kukwepa” Rais Magufuli.
Rais Magufuli
ameelezea kutofurahishwa na mrundikano wa kesi za kodi mahakamani na
ametaka tatizo hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa linasababisha kodi nyingi
kutolipwa kwa kusubiri mivutano ya kesi.
Amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji
kwa ufuatiliaji mzuri wa fedha za bajeti zinazoelekezwa katika miradi
mbalimbali na kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kuzirejesha hazina na
kuzielekeza mahali pengine zinapohitajika.
Aidha, Rais Magufuli
amemtaka Naibu Katibu wa Fedha na Mipango Mkuu Ndunguru na Naibu
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mbibo kwenda kurekebisha dosari zote zilizopo
katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana
kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya Serikali.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
amesema viongozi hao wanatarajiwa kufanya vizuri zaidi katika nafasi
walizopewa hivi sasa hasa ikizingatiwa kuwa wanakwenda kufanya kazi
katika ofisi zenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere
wamemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa viongozi hao na wameahidi
kwenda kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wa fedha za bajeti na
kufanyia kazi changamoto ya kupanua uwigo wa kodi na kuongeza idadi ya
walipa kodi.
Comments
Post a Comment