
Rais
Donald Trump amezungumza kwa simu na mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali
Khalifa Haftar, akimuahidi kumuunga mkono, licha ya jitihada za Umoja
wa Mataifa kusitisha mapigano ya kuwania udhibiti wa Tripoli.
Katika
mazungumzo hayo ya jana, Trump na Haftar walijadiliana hatua za
kupambana na ugaidi na haja ya kufikia amani na utangamano nchini Libya,
kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.
Taarifa
ya Ikulu hiyo inasema kwamba Trump alilitambuwa jukumu muhimu la
Jenerali Haftar katika kupambana na ugaidi na kulinda rasilimali ya
mafuta ya Libya.
Marekani
inaungana sasa na Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu
katika kumuunga mkono mbabe huyo wa kivita, ambaye mapambano yake ya
kutwaa madaraka yanatishia kuirejesha tena Libya kwenye mapigano ya
wenyewe kwa wenyewe.
Ikulu
ya Marekani haikusema kwa nini ilichelewa kutoa taarifa ya mazungumzo
hayo ya simu kati ya Trump na Haftar, lakini wachunguzi wanasema uamuzi
wa Trump kumsifia Haftar ni ushahidi wa kwa nini jenerali huyo muasi
amekuwa na dhamira ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, unaodhibitiwa na
serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, anayetambuliwa na
Umoja wa Mataifa.
Kamanda
huyo wa kijeshi anaunga mkono serikali hasimu ya Libya yenye makaazi
yake mashariki mwa nchi hiyo na amekataa kuyatambua mamlaka ya serikali
iliyo mjini Tripoli.
Siku
ya Alhamis (Aprili 18), Urusi na Marekani zilipinga rasimu ya azimio la
Uingereza ambalo lilikuwa likiungwa mkono na Ufaransa na Ujerumani
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka usitishwaji mapigano
nchini Libya.
Urusi
ilisisitiza kutokuwepo ukosowaji wowote dhidi ya Haftar kwenye rasimu
ya azimio hilo, huku Marekani ikitaka ipewe muda zaid kufikiria hali
ilivyo.
-DW
Comments
Post a Comment