MAGUFULI : MUDA WANGU UKIISHA NITAONDOKA TAREHE HIYO HIYO..ATAYEKUJA AJE AYAHARIBU MWENYEWE

Rais John Magufuli amesema muda wake wa uongozi ukiisha ataondoka madarakani tarehe hiyohiyo kwa kuwa yeye sio rais wa maisha.

“Mimi sio rais wa maisha ni rais wa muda, nataka niwahakikishie muda ukimalizika nitaondoka tarehe hiyohiyo ila kabla sijaondoka, maendeleo myapate kweli ili mwingine atakayekuja aje ayaharibu mwenyewe na itakuwa dhambi yake kwa Mwenyezi Mungu,” 
alisema jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Newala akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Mtwara.
“Kwa hiyo nitasimamia (nchi) kwa uadilifu mkubwa. Mafisadi wote nitalala nao mbele kwa sababu kutumbua ndio nimeanza, ukila hela ya serikali hata kama una cheo gani utaondoka tu.” 

Alisema katika kipindi chake cha uongozi maendeleo yameanza kupatikana ikiwamo ununuzi wa ndege, elimu bila malipo, umeme maji na mambo mengine.
“Kwa hiyo mmenichagua nisimamie, usimamizi ni kazi kubwa ndugu zangu, naomba tushikamane. Ninataka Tanzania iwe ya viwanda,” alisisitiza.
Aliwataka viongozi wa Mkoa wa Mtwara kusimamia viwanda vinavyoanzishwa bila kuchelewesha na kuonya asije kutokea mfanyakazi yeyote wa kuzembe katika hilo.

Comments