
Kufuatia ziara ya Naibu Waziri Nyongo soko la madini kufunguliwa Kahama
Na Greyson Mwase, Kahama
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kimadini wa Kahama inatarajia
kuanzisha soko la madini mapema ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali
kupitia Wizara ya Madini katika kudhibiti utoroshwaji wa madini.

Kutoka
kulia Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Kamishna Msaidizi-
Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali
wakisikiliza kero za wamiliki wa mitambo ya kuchenjulia dhahabu (hawapo
pichani) kupitia mkutano maalum uliofanyika Wilayani Kahama Mkoani
Shinyanga.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo aliyoifanya mapema leo tarehe 30 Machi, 2019 katika
Wilaya ya Kahama lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji na
uchenjuaji wa madini ya dhahabu, kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji wa madini.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kamishna
Msaidizi- Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali
wataalam kutoka Tume ya Madini pamoja na wawakilishi wa vyombo vya
ulinzi na usalama.
Mara baada ya kufanya ziara katika baadhi ya mitambo ya kuchenjua
dhahabu, Nyongo alifanya kikao na wamiliki wa mitambo hiyo na kusikiliza
kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Mara baada ya kusikiliza kero husika ikiwa ni pamoja na ya kutokuwepo
kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo
alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Adrea
Fabian kuhakikisha sehemu ya ofisi yake inatumika kama soko la madini ya
dhahabu ambapo wauzaji na wanunuzi watakuwa wanafanya biashara huku
serikali ikipata mapato yake, kauli ambayo ilipokelewa kwa shangwe na
wafanyabiashara wa madini ya dhahabu.
Aliendelea kusema kuwa kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya
Kahama, kunachochea utoroshwaji wa madini ya dhahabu kwakuwa inakuwa
vigumu kwa wauzaji wa madini hayo kusafiri umbali mrefu hadi Geita kwa
ajili ya kwenda kuuza madini hayo.
“Hapa tunataka kuhakikisha biashara ya madini inafanyika hapa hapa
ili kuwarahisishia wafanyabiashara wa madini ya dhahabu huku Serikali
ikipata mapato yake,” alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine, Nyongo aliutaka uongozi wa Ofisi ya Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama kushirikisha mamlaka nyingine
za Serikali kama vile Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Vyombo vya Ulinzi na
Usalama, Mabenki na soko kuanza mara moja.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wamiliki wa mitambo ya kuchenjua
dhahabu kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za madini kwa
kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini.
Wakizungumza katika nyakati tofauti wamiliki wa mitambo ya
kuchenjulia dhahabu walioshiriki katika kikao hicho mbali na kumpongeza
Naibu Waziri Nyongo wamesema kuwa uwepo wa soko hilo utawarahisishia
sana biashara ya madini kutokana na kuepukana na matapeli huku serikali
ikipata mapato yake stahiki.
Walisema kabla ya uamuzi huo wamekuwa wakisafirisha madini hadi Geita
kwa ajili ya kuuza hali inayopelekea baadhi yao kuuza kwa watu wasio
waaminifu.
Comments
Post a Comment