Chama
Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania kwa masikitiko kinauarifu umma kuhusu
tukio la kaburi la marehemu Aman Anywelwisye Kalyembe mwenye Ualbino,
aliyezikwa mwaka 2015 kufukuliwa usiku wa kuamkia tarehe 23/4/2019
katika kijiji cha Ibililo kata ya Nkunga wilayani Rungwe ambapo wahusika
waliondoka na masalia ya viungo vya marehemu.
Tukio
hili la tatu kwa mkoa wa Mbeya limeibua simanzi na hofu kwa Watu Wenye
Ualbino na familia zao, kwa uzoefu kuwa linahusishwa na imani za
kishirikina hasa kipindi hiki tunapoelekea mwaka wa uchaguzi 2020. Ni
ishara wazi ya ukatili kwa Watu Wenye Ualbino si tuu wakiwa hai bali
hata wakiwa wafu.
Chama cha watu wenye ualbino Tanzania kinaungana na wadau na wote wenye mapenzi mema kukemea vikali tukio hili ovu.
Ni
tukio ambalo limejitokeza wakati baadhi ya wenzetu wako katika vituo
maalum, huku kiu yao na jitihada za serikali na wadau wengine ikiwa ni
kuona wanarejea kuishi na familia zao, ndugu zao, marafiki na jamii zao
katika maeneo yao.
Tukio
hili linarejesha hofu kwa Watu Wenye Ualbino na familia zao kwani ni
tukio la 23 la vitendo ovu vya ukiukwaji wa heshima ya makaburi ya watu
wenye ualbino likihusishwa na imani za kishirikina.
Watu
Wenye Ualbino na familia zao watafurahi kuona serikali inachukua hatua
stahiki kwa wakati ili matokeo mazuri tuliyokuwa tumeyafikia, yakiwemo:
watoto wenye ualbino kuanza kuandikishwa shule za kawaida ndani ya
maeneo yao na vituo vingi vikiwepo Buhangija (Shinyanga) na Kabanga
(Kigoma) kuanza kupunguza idadi ya watoto na watu wazima wenye ualbino,
yawe endelevu.
Tunamwomba
Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuingilia kati suala hili, ikiwa ni kutumia nafasi yake kukemea uovu huu
na kuwezesha kifedha mikakati iliyopo na itakayokuwepo yenye nia ya
kukomesha uovu huu dhidi ya Watu Wenye Ualbino na zaidi jamii ipate
hamasa na kuziacha fikra potofu na matendo ya kishirikina.
Miongoni mwa mipango tunayoomba iwezeshwe na serikali ni pamoja na:
1.
Mpango kazi wa kutokomeza mauaji na ukatili wa watu wenye ualbino
Tanzania uliondaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa
kushirikiana na wadau wengine.
2.
‘Cross-Border Cooperation Plan on Preventing and Combating Trafficking
and the Protection of Persons with Albinism in Malawi, Tanzania and
Mozambique’ Ulioandaliwa na International Organisation for Migration
(IOM), serikali kwa uwakilishi kupitia wizara ya Mambo ya Ndani na
wadau wengine.
3.
‘Joint Programme for the Protection and Wellbeing of People with
Albinism in Tanzania’ Ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu
wa UNESCO kwa ushirikiano na wadau wengine.
4.
‘ACTION STRATEGY: Minorities and Other Vulnerable Groups’ ulioandaliwa
na Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) kwa ushirikiano na
wadau wengine.
5.
‘Regional Plan of Action on Albinism adopted on May 22, 2017 by the
African Commission on Human and Peoples' Rights’ ulioandaliwa na
mtaalamu wa kujitegemea wa UN akisimamia haki za watu wenye ualbino.
Tunaitaka
serikali katika ngazi zote wakati huu wa kuelekea chaguzi za serikali
za vijiji na mitaa na kwenye uchaguzi mkuu mwakani 2020 kuweka ajenda ya
hamasa kwa jamii kuhusu ualbino na athari za vitendo vya kishirikina
kwenye kampeni zao.
Jeshi
la Polisi limefanya kazi nzuri na ya kupongezwa kwa kipindi cha miaka
kadhaa iliyopita. Juhudi zao zimechangia kupungua kwa matukio. Mafanikio
haya yamechangiwa pia na jamii kutoa ushirikiano hivyo tunaomba mtu
yeyote mwenye taaifa yoyote kuhusiana na matukio haya afikishe jeshi la
polisi au awasiliane nasi kwa wakati ili kufanikisha kuwakamata watu
hawa waovu. Tunamsihi sana IGP Simon Sirro kuongeza kasi hasa katika
upelelezi na kushiriki katika mchakato wa kuelimisha na kuhamasisha
jamii kulinda na kuheshimu utu na uhuru wa Watu Wenye Ualbino na familia
zao.
Mahakama
zina mchango mkubwa kukomesha mauji kupitia adhabu kali ili iwe kama
elimu na fundisho kwa jamii. Watu Wenye Ualbino wana imani na Mheshimiwa
Jaji Mkuu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla
wakitarajia kwamba kesi zilizochukua muda mrefu zitashughulikiwa ziishe
kwa wakati sanjari na adhabu stahiki kutolewa kwa watakaobainika kuwa na
hatia.
Kutokana
na matukio haya, Watu Wenye Ualbino na familia zao ni vyema kuendelea
kuchukua tahadhari stahiki kwa ajili ya ulinzi wao wakati wote. Toa
taarifa polisi na au mamlaka za karibu mapema iwezekanavyo uonapo
kiashiria chochote cha uhalifu ili jitihada za kuzuia zifanikiwe.
Vyombo
vya habari, viongozi wa dini, serikali kupitia viongozi wa kisiasa,
Wizara na taaisi nyingine za kiserikali na za kiraia tuongeze juhudi
hasa katika elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali ambazo ni endelevu, hii
itasaidia sana kuibadili jamii kifikra ili hatimaye utu wa mtu mwenye
ualbino uthaminike.
Mungu ibariki Tanzania
Nemes Colman Temba
Mwenyekiti – Taifa
Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania
Aprili 27, 2019
Kwa mawasiliano
Simu (ofisi): 022 2110527
Mob. (Mwenyekiti): 0784 874 592
Email: info@tas.or.tz
Comments
Post a Comment