WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya kilimo ina nafasi kubwa ya
kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini iwapo changamoto zinazoikabili kama
za upatikanaji wa pembejeo, mbinu na miundombinu duni ya uzalishaji,
usafirishaji, uchakataji wa mazao na masokozitafanyiwa kazi kwa wakati.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Machi 19, 2019) wakati akifungua ofisi ya
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa Kanda ya Ziwa. Ameutaka
uongozi wa benki hiyo ushirikiane na wadau wengine kutatua changamoto
za kilimo nchini ili ndoto ya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na
viwanda ifikapo mwaka 2025 itimie.
Waziri Mkuu amesema bado sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea
kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa zimesababisha
ufinyu wa tija hususan kwa wakulima wadogo, hivyo amewaagiza viongozi wa
TADB waendelee na kasi ya utoaji huduma ili kuwafikia wakulima na
wafuaji wengi zaidi nchini.
“Endeleeni kufanya kazi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuweka na
kutekeleza mipango ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima,
wafugaji na wavuvi nchini. Pia panueni zaidi wigo wa huduma hususan
utoaji wa mikopo katika kuendeleza miradi ya miundombinu ya kilimo,
ufugaji na uvuvi na kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kwa lengo la
kuinua uzalishaji”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Benki Kuu ndiyomdhibiti
mkuu wa mabenki nchini inao wajibu wa kutambua umuhimu wa kuandaa kanuni
mbadala na sera za fedha ambazo ni rafiki kwa benki za mandeleo ya
kilimo na ujasiriamali.
Amesema lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma ya mikopo ya kibiashara
tena yenye kuvutia kwenye sekta ya kilimo, hivyo ameitaka Benki Kuu
iangalie namna ya kushirikiana na wadau hususan wa kilimo kuandaa kanuni
maalumu za usimamizi angalifu wa fedha ambazo zitazingatia mazingira
halisi ya kilimo na changamoto zake.
“Sambamba na kushughulikia sera au kanuni ambazo zinarahisisha kufanya
biashara katika kilimo, Benki Kuu, pia inatakiwa kuendesha zoezi hilo
bila kuhatarisha utulivu wa kifedha na kujihami na madhara na hatari
zinazoambatana na ukopeshaji”.
Nae, Naibu Waziri wa Kilimo, ….Bashingwa amesema ufunguzi wa benki hiyo
kwa Kanda ya Ziwa ni hatua nzuri ambayo inakwenda kuwasogezea huduma
wakulima, hivyo ameutaka uongozi wa benki hiyo uandae utaratibu
wakuwafundisha wakulima namna ya kuandika maandiko kwa ajili ya kuomba
mikopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine amesema
hadi kufikia Februari 28, mwaka huu benki ya TADB imefanikiwa kukuza
mtaji wake na kufikia kiasi cha sh. bilioni 68 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 13 kutoka mtaji wa sh. bilioni 60 uliotolewa na Serikali mwaka
2015.
Mkurugenzi huyo amesema ukuaji wa mtaji wa benki hiyo umechangiwa na
malimbikizo ya faida iliyotengenezwa katika kila mwaka wa fedha tangu
kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2015, kutokana na utoaji wa mikopo ya
kimkakati inayotolewa kwa wateja wao.
“Kilimo ‘kinabenkika’ kwani katika msimu wa pamba wa mwaka 2018 TADB
ilitoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha ununuzi na usambazaji wa
viuatilifu vya zao la pamba kwa wakulima katika mikoa 17 ikiwemo yote ya
Kongani ya Kanda ya Ziwa na wilaya 49 nchini”.
Amesema mkopo huo ulichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la uzalishaji,
ambapo kwa msimu wa pamba wa mwaka 2018, mavuno ya pamba yaliongezeka na
kufikia tani 221,600 ikiwa ni ongezeko la asilimia 67 ikilinganishwa na
tani 133,000 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2017.
Baada ya kufungua ofisi hiyo ya TADB kwa Kanda ya Ziwa, Waziri Mkuu
alikabidhi matrekta 16 aina ya URSUS kwa vyama vya msingi, ambapo
viongozi wa vyama hivyo wameishukuru Sekali kwa uamuzi wake wa kuwajali
wakulima kwa kuwapatia huduma muhimu zikiwemo pembejeo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Comments
Post a Comment