WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa tahadhari kwa wadau wote wa madini
kuwa atakayekamatwa anatorosha madini, atachukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.
Pia amewataka viongozi na watendaji wote wa Serikali wasimamie kwa
weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo kuhusu sekta ya
madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu
kwenda nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa tahadhari hiyo leo (Jumapili, Machi 17, 2019) wakati
akifungua soko la madini la Mkoa wa Geita. Ufunguzi wa soko hilo ni
utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilotoa tarehe
22.01.2019 la kuitaka mikoa yote ianzishe masoko ya madini.
Waziri Mkuu ameitakaWizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa,
Idara na Taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta
ya madini waheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia
vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
“Wizara ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya
utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya
kwa wachimbaji na wafanyabishara wa madini”
Waziri Mkuu ameviagizaVyombo vya Ulinzi na Usalama vihakishe soko hilo
linapata ulinzi wa kutosha muda wote ili watendaji, mali zitakazokuwemo,
vitendea kazi na miundombinu yote iwe salama muda wote. “Mkuu wa mkoa
na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nawaagiza hakikisheni Suala
hili mnaliandalia utaratibu haraka iwezekanavyo”.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuielekeza mikoa mingine yenye
kiwango kikubwa cha uzalishaji wa madini hususan ya metali na vito
iharakishe uanzishwaji wa masoko ya madini sanjari na miundombinu yote
muhimu ili masoko hayo yaanze kufanya kazi kabla ya kwisha kwa mwaka huu
wa fedha 2018/2019.
Amesema anaamini kwamba, usimamizi mzuri wa soko hilo na masoko mengine
ya madini yanayoendelea kuanzishwa nchini utaimarisha makusanyo ya kodi
za Serikali na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
Vilevile, amesema wafanyabiashara wa madini, hususan kutoka nje ya nchi
wataongezeka kwa sababu tutakuwa tumewaepusha na matapeli na vikwazo
vingine vya kibiashara. “Uimara wa soko hili pia, utaboresha uhusiano
kati ya wadau wa biashara ya madini na Serikali”.
Waziri Mkuu amesema Serikali imefuta baadhi ya tozo na kodi ambazo
zilikuwa kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo.
Miongoni mwa tozo zilizofutwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na
Kodi ya Zuio ya asilimia tano ya mwisho (final withholding tax)
inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote.
Amesema baada ya kufutwa kwa kodi na tozo hizo Serikali inatarajia kuwa
utoroshwaji wa madini utapungua, pia kutasaidia wachimbaji wadogo
kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini; kupunguza gharama
za uendeshaji wa shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa
mapato kwa nchi.
“Nitoe wito kwa wachimbaji wote wadogo kwamba endeleeni kushirikiana na
mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yenu kwa
kufuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali”.
AmesemaSerikali inachukua hatua zote hizo si kwa lengo jingine bali
kuziba mianya ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji
kodi, na hivyo, kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela
katika maeneo mengi ya nchi yetu.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vema katika kuhakikisha vikwazo
vyote vilivyomo katika mnyororo wa biashara ya madini vinaondolewa kwa
lengo la kukuza sekta hiyo na kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa
ujumla.
Amesema Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na
maendeleo ya sekta ya madini. “Utekelezaji wa dhamira hii unakwenda
sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha
kuimarika kwa sekta ya madini nchini”.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia
ukosefu wa masoko ya uhakika ya madini ambao umekuwa sababu ya
utoroshwaji madini, hivyo kuanzishwa kwa soko hili kunawahakikishia
wachimbaji wadogo masoko na kukua kwa kipato kutokana na shughuli za
madini.
Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na malalamiko ya
kudhulumiwa au kupunjwa kutoka kwa baadhi ya wachimbaji wadogo, vitendo
hivyo vimekuwa vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa
waaminifu.
“Ndugu wachimbaji wadogo, soko hili linakwenda kuwa mwarobaini wa tatizo
hilo kwani litasheheni vifaa vya kupimia uzito na ubora wa madini kabla
hayajauzwa. Naielekeza Tume ya Madini, isimamie ipasavyo vifaa na
taratibu za vipimo kwenye soko hili na kuhakikisha hakuna manung’uniko
juu ya utendaji kazi wa vifaa hivyo”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa soko hilo pia litaondoa uwezekano wa
wanunuzi wa madini kuibiwa na wajanja wachache wanaojifanya kuwa na
madini wakati hawana. “Nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko hili
kikamilifu ili kuepuka udanganyifu na matapeli”.
Pia ameiagiza Tume ya Madini kuratibu bei za madini ndani ya soko hilo
na ihakikishe mchimbaji anapata stahiki zake, Serikali inapata mapato
yake na mfanyabiashara naye ananufaika. “Tunaimani kabisa tatizo la
kudhulumiana na kupunjana linaenda kwisha kabisa. Na kwa kweli ikitokea
mtu amepunjwa, atakuwa amejitakia mwenyewe”.
“Ndani ya soko hili kutakuwa na huduma zote muhimu kwa mfanyabiashara
ikiwemo huduma za Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Mabenki na nyinginezo, hivyo kuokoa muda na gharama nyingine katika
kuendesha biashara hii ya madini.
Amesema soko hilo litasaidia sana katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali na takwimu za biashara ya madini. Hivyo, niwasihi wachimbaji wa
madini kulitumia soko hili na kuacha vitendo vya utoroshaji wa madini.
Serikali kwa upande wake, haitomvumilia mtu yeyote yule atakaye
jihusisha na utoroshaji wa madini.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri wa
Nishati Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Costantine Kanyasu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon
Msanjila, Wabunge wa mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robertt Gabriel, wakuu wa mikoa jirani na maafisa wa Serikali.
Comments
Post a Comment