WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza
Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mwanza ihakikishe inafanya msako wa
watu wote waliohusika na wizi wa fedha na vifaa katika eneo la ujenzi wa
mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika mji wa Misungwi mkoani
Mwanza.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi
19, 2019) wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa Maji na Usafi wa
Mazingira uliopo wilayani Misungwi, ambapo ametumia fursa hiyo kuiagiza
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mwanza iimarishe ulinzi katika
eneo la mradi huo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya
kupokea taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya uvamizi wa mara kwa mara
kwenye eneo hilo la mradi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Nyahiti
wilayani Misungwi, Mwanza.
“Hawa waliofanya tukio hilo la uvamizi
katika eneo la mradi si tu wanamuhujumu mkandarasi na kampuni yake, bali
wanahujumu jitihada za Serikali ili miradi ya maendeleo kwa wananchi
isikamilike hatutakubali, wananchi tushirikiane katika kuwabaini wote
waliohusika.”
Ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa
Misungwi ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 inayoelekeza Serikali
kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 95 wakazi waishio
mijini na waishio vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.
Awali,Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa amesema ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Misungwi
unatekelezwa kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Huduma za Majisafi na Usafi
wa Mazingira ya Ziwa Viktoria, ambao unatekelezwa katika miji ya
Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro
milioni 104.5 sawa na wastani wa sh. bilioni 276.
Amesema katika kiasi hicho cha fedha,
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) pamoja na Benki ya Uwekezaji ya
Ulaya (EIB) zinachangia Euro milioni 90 sawa na sh. bilioni 238 ambazo
ni mkopo wa masharti nafuu, ambapo Serikali ya Tanzania inachangia Euro
milioni 14.5 sawa na sh. bilioni 38.
Profesa Mbarawa amesema mradi wa maji na
usafi wa mazingira katika mji wa Misungwi unagharimu kiasi cha Euro
milioni 4.85 ambazo ni sawa na wastani wa sh. bilioni 12.85 ambazo
zinatumika katika ujenzi wa kituo cha uzalishaji na kutibu maji, ulazaji
wa mabomba kwa umbali wa kilomita 53.7.
Pia, fedha hizo zitatumika kwenye ujenzi
wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ukubwa wa lita 600,000 na
lita 300,000, ujenzi wa kituo cha kutibu majitaka, ununuzi wa magari
mawili moja la kunyonya majitaka na Toyota pick up na pikipiki mbili
pamoja na ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya Maji na nyumba mbili za
watumishi katika kituo cha uzalishaji.
Waziri Profesa Mbarawa amesema mbali na
ujenzi huo pia watajenga maabara ya kupima ubora wa maji na karakana ya
matengenezo. Mradi huo pia utaunganisha kaya 2,158 katika mfumo wa maji
pamoja na kuwafungia mita za maji na ujenzi wa vituo 13 vya kuchotea
maji.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya M/S
China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) ya China chini
ya Mhandisi Mshauri Kampuni ya Egis ya Ufaransa na unasimamiwa na
Mamlaka ya Maji Jijini Mwanza (MWAUWASA) ulianza Mei, 2017 na
unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Comments
Post a Comment