Waziri Biteko Azindua Bodi Ya Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Aitaka Kuiwezesha GST Kurahisisha Maisha Ya Wachimbaji
Bodi
ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imetakiwa
kuiwezesha taasisi hiyo kurahisisha maisha ya Wachimbaji Wadogo, wa Kati
na Wakubwa kwa kuhakikisha wanapata taarifa za tafiti zinazofanywa na
taasisi hiyo.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizundua Bodi ya GST
na kueleza kuwa, shughuli za utafiti ni moja ya maeneo muhimu katika
sekta ya madini kutokana na kutoa uhakika kwa wachimbaji na hivyo
kukidhi matarajio ya wadau.
Pia,
ameitaka bodi kuiwezesha taasisi hiyo kutoa ubunifu mpya utakaowezesha
taasisi hiyo kuongeza mapato kwa serikali kutokana na shughuli na huduma
zinazotolewa na GST.
Katika
hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka bodi hiyo kuhakikisha GST
inapata Ithibati ya maabara yake ikiwemo kutangaza huduma zinazotolewa
na maabara hiyo ili kuwawezesha wadau kuifahamu na kuitumia.
Aidha,
ameitaka bodi husika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera,
sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kwamba, taasisi hiyo inao
watendaji wazuri wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kiamilifu na
kutumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST Yokberth
Myumbilwa, kwa kusimamia vema utendaji wa GST.
Naye,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema taasisi hiyo ni kitovu
cha sekta ya madini nchini na kwamba ndiyo imeshikilia mstakabali wa
wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.
Ameongeza
kuwa, bado yapo majukumu ya taasisi hiyo ambayo hayajafanikiwa na hivyo
kuitaka bodi hiyo chini ya Prof. Ikungula kuhakikisha yanafanikiwa.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingura amesema
bodi hiyo inatambua umuhimu wa rasilimali madini katika kuchangia pato
na kukuza uchumi wa taifa ikiwemo kutambua nia na lengo la Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Magufuli.
Amesema
ili kufikia lengo hilo, ni muhimu GST ikawezeshwa ipasavyo kupitia
wizara ili iongeze kasi na tija zaidi katika kutekeleza majukumu yake,
hususan katika maeneo ya kufanya utafiti na kukusanya taarifa muhimu za
kijiosayansi za kubaini maeneo yenye miamba yenye vishiria vyakuwepo
madini ya kimkakati yanayohitajika zaidi katika matumizi ya teknolojia
ya viwanda vya kielekitroniki, zana za utafiti wa mawasala ya anga na
matumizi maalum katika viwanda vingine, ili kuvutia uwekezaji wa ndani
na nje ya nchini katika maeneo hayo.
“Kwa
mfano madini lithium, cobalt na palladium yanazidi kupata umuhimu wa
pekee katika matumizi ya viwanda vya kimkakati. Hivi majuzi takriba wiki
moja iliyopita bei ya Palladium ilifikia kiasi cha dola za kimarekani
1,600 kwa wakia na kuzidi hata dhahabu ambayo ikiwa karibu dola 1,300
kwa wakia moja. Lakini si wengi wanatambua madini ya Palladium ambayo
yako katika kundi la metali za Platinum, yaani Platinum Group Metals
(PGM),” amesisitiza Prof. Ikingura.
Ameongeza
kuwa, eneo jingine ni uboreshaji wa huduma za maabara za uchunguzi na
upimaji wa miamba na madini yake ili zikidhi viwango vya kimataifa, na
hivyo kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kutumia zaidi maabara za
ndani ya nchini badala ya kupeleka sampuli katika maabara za nje ya
nchi, na hivyo kupoteza fedha za kigeni.
Vilevile,
amesema ipo haja ya kuboresha na kuongeza thamani taarifa za jiofikizia
na jiokemia zilizo katika hifadhi au kanzidata ya GST ili ziweze kuwa
na thamani kubwa zaidi kwa taifa na kwa wawekezaji katika sekta ya
madini, suala ambalo litaiweesha GST kuongeza maduhuli ya serikali
kupitia wizara.
Mbali
ya Mwenyekiti, wajumbe wa bodi hiyo ni Abdulkarim Hamisi Mruma, Emanuel
Mpawe Tutuba, Bibi Bertha Ricky Sambo, Shukrani Manya, David R. Mulabwa
na Bibi Monica Otaru.
Bodi hiyo imezinduliwa Machi 27, 2019 Makao Makuu ya GST, jijini Dodoma.
Comments
Post a Comment