Watu 24 wamepoteza maisha mashariki mwa Zimbabwe, baada ya kukumbwa na
kimbunga Idai kilichoambatana na mvua kubwa. Kimbunga Idai tayari
kimesababisha vifo zaidi ya 100 katika nchi za Msumbiji na Malawi.
Kiasi ya watu wengine 40 hawajulikani walipo nchini Zimbabwe,
amearifu waziri wa mawasiliano kupitia ukurasa wa twitter. Nyumba, mitaa
na mashamba vimeathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua.
Wahudumu
wa uokoaji wanajaribu kulifikia eneo lililoathirika zaidi la
Chimanimani karibu na mpaka na Msumbiji, lakini hata hivyo zoezi hilo
limetatizika kutokana na madaraja kusombwa na maji. Takribani wakazi
500,000 katika mji wa Beira wameathirika baada ya mawasiliano na huduma
ya umeme kukatika.
Mashirika ya misaada yana hofu kwamba maelfu
ya watu watakosa makaazi baada ya kimbunga hicho. Nchi za Msumbiji,
Malawi na Zimbabwe ndizo zilizoathirika zaidi na kimbunga Idai. Zaidi ya
wakaazi milioni 1.5 katika mataifa hayo matatu, kulingana na maafisa wa
serikali na Umoja wa Mataifa.

Maeneo yaliyoathirika na kimbunga Idai
Watu
70 wamejeruhiwa vibaya, kwa mujibu wa gavana wa jimbo lililoathirika la
Sofala Albert Mondlane. Mji mwingine wa bandari wa Beira nchini
Msumbiji nao umeathirika na kimbunga Idai ambapo uwanja wa ndege
ulifungwa, umeme kukatwa na makazi mengi kuharibiwa. Kimbunga hicho
kilianzia Beira Alhamis jioni na kuenea hadi maeneo ya mipakani ya
Zimbabwe na Malawi.
Shule na hospitali pamoja na vituo vya polisi
navyo vimeharibiwa sana. Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na
lile la msalaba mwekundu wanaendelea kutoa msaada katika juhudi za
uokoaji pamoja na kusambaza misaada ya chakula na dawa.
Rais wa
Msumbiji Filipe Nyusi amesema uharibifu unatia wasiwasi na kwamba
mafuriko yametatiza ndege kutua kuendelea na shughuli ya uokozi. Msemaji
wa serikali ya Zimbabwe Nick Mangwana amesema hii leo kwamba watu 24
wamepoteza maisha hususan katika eneo lililoathirika zaidi la
Chimanimani.
Televisheni ya Zimbabwe ZBC imeripoti kuwa watu 150
hawajulikani walipo. Jeshi la Afrika Kusini limetuma ndege na wataalamu
10 wa afya kusaidia Msumbiji na Malawi.
Comments
Post a Comment