Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel amewataka wananchi hususan wafugaji kutotumia matamko ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli vibaya kwa
kutafuta mianya ya kutolipa kodi.
Prof.
Gabriel amebainisha hayo akiwa katika mnada wa upili wa Meserani uliopo
wilaya ya Monduli Mkoani Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua
utendaji kazi wa watumishi waliopo katika mnada huo na kusikiliza kero
za wafugaji.
Akizungumza
na wananchi mara baada ya kufanya ziara hiyo Prof. Gabriel amesema
Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwezi mmoja itashirikiana
na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kutoa tafsiri sahihi ya
mfanyabiashara mdogo anayestahili kukatiwa kitambulisho cha biashara
ndogo ndogo (machinga) cha Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka,
kilichotolewa na Rais Magufuli kutokana baadhi ya wafugaji kutaka
kufahamu endapo wanastahili kupatiwa vitambulisho.
“Mheshimiwa
rais alikuwa amelenga hasa wale wafanyabiashara wadogo wadogo na
tunachoamini tutaendelea kulifanyia kazi lakini suala la machinga kwamba
naye mfanyabiashara wa ng’ombe kuhusishwa katika sifa za mfanyabiashara
ndogondogo bado ni gumu kulitolea majibu, lakini ushauri tusitumie
matamko ya rais vibaya tusitafute kichaka cha kujificha kwamba nawe ni
machinga, wewe mwenyewe fikiria na jitafakari tulipe kodi na tujenge
nchi yetu.” Alisema Prof. Gabriel
Akizungumza
na wafugaji hao Prof. Gabriel amepokea kilio cha wafugaji kuwa wamekuwa
wakiuza ng’ombe kwa makadirio au matakwa ya mnunuzi kutokana na
kutokuwepo kwa mizani ili waweze kuuza ng’ombe kwa kilo badala ya bei ya
kukadiria kati ya mfugaji na mnunuzi wa ng’ombe, kitendo ambacho
wafugaji hao wamesema kimekuwa kikiwafanya wasiuze mifugo yao kwa bei
yenye tija kwao.
“Lengo
letu ni kuhakikisha minada yote hasa ya upili na ile ya mipakani
inatumia mizani, mnada wa Kimesera mzani wake uko tayari unatakiwa
kufanyiwa marekebisho ili kuondokana na bei ya kukisia katika kipindi
cha mwezi mmoja.” Alisema Prof. Gabriel
Aidha
katibu mkuu huyo, amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuhakikisha
wanawapatia ng’ombe malisho bora ili wapate mazao bora ya mifugo yao
huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikihakikisha inaendelea kuimarisha
matibabu ili mifugo iwe na afya bora.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel amesema pia licha ya uwepo wa masoko ya mifugo hususan
ng’ombe hapa nchini, wizara inajikita katika kutafuta masoko ya mifugo
nje ya nchi.
“Tunachoangalia
hivi sasa ni kuangalia na masoko ya nje ya nchi lakini hauwezi kuuza
ng’ombe nje ya nchi ambaye hana afya bora na tunaamini tukiendelea hivi
hata mchango wetu wa wizara kwenye uchumi wa viwanda utakuwa ni mzuri.”
Alisema Prof. Gabriel
Naye
Bw. Kandidi Mlinyi ambaye ni msimamizi wa mnada wa Meserani amesema
kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika
ukanda wa Wilaya ya Monduli hivyo kuwa na mazingira magumu ya
upatikanaji wa huduma hiyo mnadani.
Kauli
hiyo imeungwa mkono na baadhi ya wafugaji ambao wamesema ng’ombe
wanaposafirishwa kutoka maeneo mbalimbali kuja katika mnada huo, kwa
wastani wanakunywa maji lita 20 hadi 60 lakini kutokana na ukosefu wa
maji ng’ombe wanakuwa katika mazingira magumu hali inayosababisha
ng’ombe hao kuchoka kwa kuwa wanapoteza maji mengi mwilini.
Katika
ziara hiyo ya Katibu Mkuu Prof. Gabriel wafugaji wamepongeza utendaji
kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwa viongozi na watendaji wa
wizara wamekuwa wakifika mara kwa mara kwa wananchi wakiwemo wafugaji
ili kutatua kero zao.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka katika uongozi wa mnada wa Meserani kwa siku
zaidi ya ng’ombe 500 huuzwa na kusafirishwa kwenda katika mikoa
mbalimbali wakati wa msimu ambao unakuwa na ng’ombe wengi kuanzia mwezi
Machi hadi Julai kila mwaka.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Comments
Post a Comment