UVCCM DAR WAZINDUA KAMPENI YA "DAR YA KIJANI" KURUDISHA MITAA NA MAJIMBO YALIYOCHUKULIWA NA UPINZANI
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dar es Salaam,
umezindua kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’ iliyolenga kurudisha
mitaa na majimbo yanayoongozwa na vyama vya upinzani.
Pamoja na mambo mengine, kampeni hiyo inalenga kuweka mikakati kuanzia
ngazi za jumuiya zote za mkoa huo, kuanza kujipanga kuelekea kwenye
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na
Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Akizugumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Chuo Kikuu
Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa
Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa kampeni hiyo itachochea
ustawi zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuzidi kukita mizizi
katika ngazi zote kuanzia mkoa hadi majimbo, wilaya hadi kata, na
matawi hadi mitaa.
“Kampeni yetu ya Dar ya Kijani kuelekea serikali za mitaa 2019, ni
kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM mitaa iliyopotea katika
uchaguzi uliopita ambayo kwayo itatusaidia kupata ushindi mkubwa kimkoa
katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa udiwani, ubunge na urais.
“Sote ni mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 wa Serikali
za Mitaa na ule Mkuu wa 2015 tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na majimbo
yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM na sababu za kupoteza huko
zinajulikana, sina haja ya kuzirejea sasa.
Hivyo sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya chama
chetu, na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza
malengo ya uwepo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola,” amesema
Kilakala.
Aidha, amesema kampeni hiyo itashuka katika wilaya, kata na matawi yote
jijini Dar es Salaam, ili kuhakikisha kila Kijana wa UVCCM anawajibika
ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani yaani Dar es
Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati wa
uchaguzi tuvune wapiga kura wa kutosha.
Naye Katibu wa UVCCM mkoa wa Dar es salaam, Mwalimu Raymond Mwangwala
aliwataka vijana nchini kuacha tabia ya kuwa wabeba pochi za watu, na
kuomba nafasi za uongozi kuanzia ngazi za serikali za mitaa kwenye
uchaguzi utakaofanyika mwaka huu 2019.
Alisisitiza Dar es salaam lazima iwe mfano na vijana watoke na kuwa
sehemu ya Historia ya Ujenzi wa Taifa la Tanzania chini ya Jemedari mkuu
na Mzalendo, Rais John Joseph Magufuli.
Mwangwala alitoa rai kwa mikoa yote kuiga kampeni za namna hiyo
zinazojenga Ari, hamasa na moyo wa kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Aliwakumbusha Vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuendesha
kampeni mbalimbali lakini kujibia upotoshwaji unaofanywa na upinzani
kila kunapokucha huku akiwataka vijana kufanya tafiti ili kusaidia
kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali.
Comments
Post a Comment