Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imezifungia simu 1,682,667 zilizokuwa zikitumika kwenye mitandao
mbalimbali ambazo zilibainika kutokuwa na sifa zikiwamo kutofikia
viwango vinavyotakiwa, zilizoibwa na zilizoripotiwa kupotea.
Takwimu hizo zitolewa jana na Mkurugenzi
wa TCRA, James Kilaba wakati akiwasilisha taarifa juu utendaji kazi wa
Mfumo wa Kuratibu na Kusimamia Mawasiliano ya Simu(TTMS) kwa wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) waliotembelea
ofisi za mamlaka hiyo.
Alisema kasoro za simu hizo zimebainika
kupitia mtambo wa TTMS ambao pamoja na mambo mengine ina moduli ya
CEIR(Central Equipment Identifications Register) ambayo ina kipengele
cha kutambua taarifa za laini za simu(sim card profile) na namba
tambulishi za mawasiliano.
“Moduli ya CEIR imewezesha kuzifungia
simu 1,682,667 zilizokuwa zikitumika kwenye mitandao mbalimbali, idadi
hii inajumuisha simu zilizobainika kutofikia viwango vinavyotakiwa,
simu zilizonakiliwa namba tambulishi(IMEI) pamoja na zile zilizoropitiwa
kuibwa ama kupotea,” alisema Kilaba.
Alisema mtambo huo pia umewezesha
kubaini mawasiliano ya simu za kimataifa zinazoingia kwa ulaghai ambako
mpaka sasa yamepungua na kufikia chini ya asilimia 10 kwa mwaka jana
kutoka asilimia 65 mwaka 2013.
Alisema mfumo huo umeonyesha miamala
ya fedha iliyofanywa na kampuni za simu ambayo imefikia Sh bilioni
8.9 kutoka Novemba 2014 hadi Februari 2019 ilyozalisha faida ya Sh
trilioni 2.5.
Kilaba alisema mfumo huo pia unatoa
takwimu za huduma za mawasiliano ya simu za sauti, matumizi ya data na
ujumbe mfupi pamoja na fedha zinazopatikana katika kila kampuni ya simu
kupitia miamala ya fedha na upigaji wa simu.
Comments
Post a Comment