
Wizara ya Serikali za Mitaa na Maendeleo ya Vijijini ya Botswana
imetangaza kuanza kutoa chakula cha asubuhi kwa wanafunzi wa shule za
chekechea na shule za msingi nchini humo kuanzia mwezi ujao.
Tangazo hilo ambalo limeelezwa kuwa ni la haraka, limetolewa Machi 18
ambapo linasema kuwa wanafunzi hao wataanza kupewa bure chakula cha
asubuhi kuanzia April Mosi kwaajili ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Serikali ya Botswana imefikia uamuzi huo kutokana na mapendekezo
yaliyotolewa na timu iliyoundwa mwaka 2013 kuwa wanafunzi wanatakiwa
kupewa vyakula vyenye virutubisho ili kulinda afya zao, ukuaji na
maendeleo pamoja na kupunguza magonjwa yatokanayo na upungufu wa lishe
bora.
Chakula ambacho kinatarajia kutolewa ni pamoja na chai, mkate, 'peanut
butter', mayai yaliyochemshwa, uji, maziwa, machungwa na 'apple'.
Chakula hicho kimependekezwa kutokana na mahitaji ya virutubisho kwa
wanafunzi, ambapo kitatolewa kwa wanafunzi hao kila siku asubuhi kabla
ya kuanza masomo.
Comments
Post a Comment