Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 16 Machi, 2019 amefanya ziara ya
kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza
wa gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam na kuagiza mradi huo
ukabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo
baada ya kubaini kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeshindwa
kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya Serikali kutoa shilingi
Bilioni 10 za ujenzi.
Ametaka wataalamu wa TBA waliokuwa wakisimamia mradi huo pamoja na Askari Magereza waondoke na kuwapisha JWTZ.
“Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA,
nisimuone mtu wa Magereza kuja kusimamia, muwaache Jeshi la Wananchi
wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi
Magereza, kwa hiyo watu wa TBA kuanzia leo nimewafukuza hapa” amesema
Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameelezea
kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika mradio huo ambao ulianza
zaidi ya miaka 2 iliyopita kwa kushirikisha Jeshi la Magereza ambalo
lilikuwa linaisadia TBA katika kazi za ujenzi, na ametaka TBA na Jeshi
la Magereza wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nataka kila mlipo watu wa Magereza
mfanye kazi, msimamie watu, kama ni ng’ombe muwafuge vizuri wazalishe
vizuri hadi muuze mazao nje, kama ni kilimo mlime kwelikweli, muwe ni
jeshi la kuzalisha, hii ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja
kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnakaa nyinyi, mlitakiwa muwe
mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofari,
tuanze kujenga” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) Kanali Charles Mbuge amesema JKT itakamilisha ujenzi huo
ndani ya kipindi cha miezi 2 na nusu kuanzia kesho na kwamba kazi
zitafanywa usiku na mchana.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka TBA
kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha shilingi
Bilioni 10 zilivyotumika, na ameonya kuwa endapo itabainika matumizi ya
fedha hizo hayaendani na kazi zilizofanyika hatua kali zitachukuliwa.
Katika mradi huo, ujenzi wa majengo 12
ya makazi ya Askari Magereza yaliyopangwa kuwa na ghorofa 4 kila moja
ulioanza Desemba 2016 umefikia asilimia 45 tu na unaendelea kwa
kusuasua.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli
amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi
wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam na kuelezea kusikitishwa na hali
ya kusuasua kwa ujenzi huo ulioanza Aprili 2017.
Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia ujenzi wa
majengo yenye ghorofa 3 ukiwa umefikia asilimia 36 na kazi za ujenzi
zikiwa zimesimama kwa muda usiojulikana.
Mmoja wa wananchi wanaosubiri kukamilika
kwa ujenzi wa nyumba hizo Mzee Omary Mpimbila amemueleza Mhe. Rais
Magufuli kuwa wamekuwa wakifanya juhudi za kufuatilia hatma ya majengo
hayo kutoka TBA na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano lakini
mpaka sasa hawajapatiwa majibu ya sababu za kutelekezwa kwake.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuchukua
hatua za haraka kuhakikisha ujenzi huo unaendelea na wakazi wa Magomeni
Kota wanapatiwa makazi kama walivyoahidiwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Machi, 2019
Comments
Post a Comment