MAOFISA USTAWI WA JAMII SHINYANGA WATINGA GEREZANI KUSHEREHEKEA SIKU YA USTAWI WA JAMII

Maofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha Siku ya Ustawi wa Jamii kwa kutembelea wafungwa wanawake katika gereza la Shinyanga,kutoa chakula kwa kaya maskini na kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto kwa wanafunzi.



Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mkoani leo Machi 21,2019 ,Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa, Lidya Kwezigabo, alisema wameamua kutembelea wafungwa wanawake kwenye gereza la Mjini Shinyanga ambao wamefungwa na watoto wao, ili kutoa elimu ya ulinzi wa mtoto na kuweza kupata haki zao za msingi.

Alisema mbali na kutembelea wafungwa hao, pia wameona ni vyema kwenda kutoa elimu ya ukatili na kujitambua kwa wanafunzi mashuleni kwani wanafunzi ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo hivyo, lengo likiwa ni kutokomeza matukio hayo ndani ya jamii.

“Sisi Maofisa Ustawi wa Jamii mkoa Shinyanga kwa pamoja tumeamua kuadhimisha siku yetu hii kwa kutoa elimu zaidi juu ya kutomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili waweze kupata haki zao za msingi ikiwamo kutimiza malengo yao ya kielimu,”alisema Kwezigabo.

“Pamoja na kutoa elimu ya ukatili pia tumetoa msaada wa sabuni za kufulia, kuogea na dawa za mswaki kwa wanawake ambao wamefungwa kwenye Magereza ya Shinyanga pamoja na msaada wa chakula kwenye kaya maskini iliyopo kata ya Mwasele katika Manispaa ya Shinyanga,”aliongeza.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Elizabeth Mweyo aliwataka wanafunzi hao pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ama mwenzao, wawe wanatoa taarifa kwa walimu au viongozi wa Serikali ili waweze kusaidiwa na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

Pia aliwataka kuacha kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi wakiwa bado wanafunzi na kutopenda vitu vya dezo ikiwamo Lifti, vitu ambavyo vimekuwa vikiwaingiza kwenye vishawishi na kujikuta wakiambulia kupewa ujauzito na kuachishwa masomo yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Sekondari Chamaguha ambayo ilitembelewa na Maofisa  Ustawi wa Jamii Abdalla Lidyati, alipongeza utolewaji wa elimu hiyo ya ukatili na kujitambua kwa wanafunzi hali ambayo itasaidia kuondokana na mimba mashuleni.

Comments