SERIKALI
imewaagiza wataalam wa mifugo wa halmashauri zote nchini kutoka
ofisini na kwenda kutoa Elimu kwa wafugaji juu ya utumiaji wa mbegu
bora za ng'ombe zinazozalishwa na kituo cha Taifa cha Uhimilishaji
Mifugo kwa njia ya chupa NAIC kilichopo Arumeru, Mkoani Arusha.
Agizo
hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Migugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.
Elisante Ole Gabriel alipokuwa akitoa Taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Kilimo, Mifugo, na Maji walipotembelea kituo hicho Jijini
Arusha.
Prof.
Gabriel, alisema kuwa ili kuendana na azma ya serikali ya uchumi wa
viwanda, ni lazima wafugaji nchini wabadilike na kuanza kufuga kwa tija
kwa ajili ya kupata nyama bora, maziwa, ngozi na Kwato, ambapo
malighafi hizo zitakidhi mahitaji ya viwanda hapa nchini.
Aidha,
Katibu Mkuu Mifugo ametoa agizo hilo kufuatia idadi ndogo ya wafugaji
waliopewa elimu mwaka 2017/2018 kuwa hairidhishi hivyo kuna kila
sababu ya watendaji wa halmashauri wanaohusika na idara ya mifugo kutoka
ofisini na kwenda kutoa elimu kwa wafugaji ili wabadilike na kufuga
kisasa.
Katibu
Mkuu aliieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa
kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 ni wafugaji Elfu 58 pekee ndiyo
waliopewa elimu ya uhimilishaji katika kituo cha NAIC ambacho ni cha
kwanza katika Bara la Afrika kwa ubora, kikizalisha mbegu Elfu 60 kwa
mwaka ukilinganisha na mahitaji halisi ambayo ni Elfu 50 kwa mwaka.
"Idadi
ya wafugaji waliopewa elimu ni ndogo na mwitikio wa utumiaji wa mbegu
hizi hauridhishi, wakati kituo kinazalisha mbegu za kutosha kwa mahitaji
ya wafugaji wote nchini, hivyo nawaagiza wataalamu wote watoke ofisini
waende kwa wafugaji kutoa elimu juu ya utumiaji wa mbegu hizi." Alisema
Prof. Gabriel.
Pia,
Prof. Gabriel alitumia fursa hiyo kuwataka wafugaji wote nchini
kuondokana na dhana potofu kuwa mbegu za chupa zinaharibu kizazi cha
Ng'ombe, jambo ambalo sio sahihi na kuwataka kutumia mbegu hizo ili
kuondokana na ufugaji wa mifugo mingi ambayo haina tija.
Naye
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema hali ya
usambazaji wa mbegu hizo kwenye vituo vilivyopo kanda saba nchini
hairidhishi kutokana na baadhi ya waataalamu kutotimiza wajibu wao wa
utoaji elimu kwa wafugaji.
"Serikali
inauza mbegu hizi kwa ruzuku ili wafugaji wasiokuwa na uwezo waweze
kumudu gharama ya Shilingi Tano kwa dozi ya mbegu moja, lakini kuna
baadhi ya wataalamu wananunua mbegu hizi na kuziuza kwa bei kubwa kati
ya Shilingi Elfu 15 na Elfu 40 huku halmashauri zikifumbia macho hali
hiyo inayosababisha mbegu kutonunuliwa kwa wingi." Alisema Naibu Waziri
Ulega.
Aidha
aliwataka wafanyabishara binafsi wanaoagiza mbegu hizo za chupa kutoka
nje ya nchi na kuwauzia wafugaji kwa bei ya Shilingi 50 hadi Laki
Moja waache mara moja, badala yake wanunue mbegu kutoka NAIC kwa sababu
mbegu hizo ni bora.
"Serikali
katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ilitenga fedha kwa ajili ya
kununua madume bora 28 kutoka nchi za nje, lengo likiwa ni kuwezesha
wafugaji kupata mbegu bora na kisasa, hivyo hakuna sababu ya kununua
mbegu kutoka nje ya nchi."Alisema.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo, na Maji Mhe. Mahamoud Mgimwa, amesema utumiaji wa mbegu hizo
utawezesha wafugaji kufuga kwa tija na kupata soko la uhakika la bidhaa
za mifugo ndani na nje ya Nchi.
"Kikubwa
hapa wafugaji wabadilike kutoka kwenye ufugaji wa mazoea na kufuga
kisasa kwa kutumia mbegu hizi za NAIC ili tushiriki uzalishaji wa
malighafi za viwanda vyetu vinavyoanzishwa kwa wingi hapa
nchini."Alisema.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
21.03.2019
Comments
Post a Comment