
Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Waziri
wa Madini Doto Biteko katikati akipitia jambo wakati wa kikao kazi cha
kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha
Jemolojia Tanzania (TGC). Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Simon Msanjila.
Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 23, jijini Dodoma wakati akifungua
kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa
Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) iliyoandaliwa na
Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Aidha, amezitaka taasisi hizo kuhama katika mtindo wa kutegemea
ruzuku ya serikali badala yake zijiendeshe kibiashara na kuwataka
watendaji wa wizara na taasisi kuhakikisha wanafanya mageuzi
yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi sambamba na kasi yake ya
ukuaji kiuchumi.
“ Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi makubwa. Tunataka
Idara, kitengo na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi ambayo
mfanyakazi anaweza kueleza amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri
Biteko.
Pia, ameongeza kuwa, ukataji madini ni suala ambalo linalopaswa
kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kutokana na umuhimu wake katika
biashara ya madini na hususan kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza
shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini ikiwemo
kuhamasisha ujenzi wa viwanda hivyo.
Vilevile, amewataka washiriki wa kikao hicho kuwasilisha mawazo
chanya yatakayosaidia kuboresha mkakati huo utakopelekea uboreshaji wa
kituo cha TGC.
Aidha, amewataka watendaji wa Kituo cha TGC kuhakikisha wanakitangaza
kituo hicho ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa madini kuwa marafiki
wa kituo hicho.
Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema
serikali iliona umuhimu wa Kituo cha TGC hali ambayo imepelekea
kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza kuwa uwepo wake unapaswa kutoa
mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika eneo la uongezaji
thamani madini.

Waziri
wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akifungua kikao kazi cha
kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha
Jemolojia Tanzania (TGC). Wengine ni watendaji wa Wizara na Taasisi.
Ameongeza kuwa, uongezaji thamani madini ni jambo ambalo serikali
inaliangalia kwa umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni mwa mambo
yaliyopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 na 2017 ili taifa liweze kunufaika zaidi .
Ameeleza masuala mengine yaliyopelekea serikali kufanya mabadiliko ya
sheria ya madini ni pamoja na kutaka kuongeza mapato ya serikali
yanayotokana na madini, serikali kushiriki katika uchumi wa madini na
kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika miradi ya madini na kampuni za
madini kushirikiana na jamii.
Aidha, amewashukuru wataalam washauri Prof. Beatus Kundi na Prof.
Marcellina Chijoriga kutokana na ushauri wao walioutoa kwa wizara wakati
wa kupitia Mikakati hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini, Prof. Simon Msanjila
amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha kila mmoja anaangalia eneo
linalomhusu katika kituo hicho na kulifanyia kazi kikamilifu ili kufikia
lengo linalotarajiwa .
Wizara ya Madini iliona umuhimu wa kukiimarisha Kituo cha TGC ili
kijiendeshe kibiashara kutokana na fursa zilizopo katika sekta ya madini
hususan kwenye ukataji wa madini. Pia, kutokana na fursa zilizopo
katika ukataji wa madini ya vito na jimolojia kwa ujumla, wizara iliona
TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo kuongeza mapato kwa
serikali.
Kazi ya kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi
Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na kuandaliwa na Wataalam
Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof.
Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es
Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizarani na taasisi zake.
Comments
Post a Comment