
Askari Polisi, PC Donald Motoulaya (29)
wa ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, amekutwa amefariki dunia
akiwa kwenye baa iitwayo Friends Pub iliyopo Manispaa ya Songea mkoani
humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma, ACP Simon Marwa
alisema tukio hilo limetokea Machi 13,2019 saa 4:30 usiku.
Kamanda Marwa alisema Motoulaya kabla ya kufariki dunia, alianguka kwenye ngazi za mlango wa baa hiyo baada ya kujikwaa.
Kamanda huyo alisema mhudumu
aliyejulikana kwa jina la Jaibu Nyoni (26), alimtoa nje na alifika
kwenye Baa hiyo akitokea Baa ya karibu aliyoitaja kwa jina la Yapenda au
Mtini pub kwa lengo kujipatia kinywaji zaidi.
“Baada ya kutolewa nje huku mhudumu
akiendelea na shughuli zake, askari huyo alijipenyeza na kuingia kwenye
chumba cha ndani cha baa hiyo na kwenda kukaa eneo lililowekwa makochi.
Huyu askari alikuwa ameyazoea mazingira ya baa hiyo, hivyo alikaa huko
bila wahudumu kufahamu kama yupo,” alisema kamanda huyo.
Walibaini kuwa kuna mtu ndani kwenye kochi na amelala asubuhi walipokuwa wanafanya usafi.
Kamanda Marwa alisema wahudumu hao
waliingiwa na hofu baada ya kumuita lakini hakuitika wala kuamka, ndipo
wakaamua kutoa taarifa kituo kuu cha polisi cha mjini Songea.
Na polisi walipofika wakabaini kuwa
askari huyo alikuwa amefariki dunia na kuuchukua mwili wake kwenda
kuuhifadhi Hospotali ya Songea (Homso).
Comments
Post a Comment