
Watuhumiwa 12 wakiwemo wafanyabishara wanne na Askari Polisi nane
waliohusika na utoroshaji wa madini ya dhahabu kilo 319.59 yenye thamani
ya shillingi bilioni 27 kinyume na sheria ya usafirishaji wa madini
nchini, leo wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa
Mwanza.
Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2019 ya uhujumu uchumi, rushwa pamoja na
utakatishaji fedha inayowakabili watuhumiwa kumi na mbili wakiwemo
wafanyabishara wanne na askari polisi nane, ambapo leo hii ikiwa ni
mara ya 3 wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa
Mwanza na kutajwa na hakimu mkazi Gwai Sumayi.
Akizungumza nje ya Mahakama wakili wa utetezi Steven Makwega anaewatetea
watuhumiwa namba 1 hadi 12 ameiomba mahakama kufuata kalenda ya
mahakama kutokana na kesi hiyo kutotajwa Februari 25 kama ilivyokuwa
imepangwa.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Gwayi Sumayi, ametaka kuwepo mawasiliano
baina ya wakili wa serikali na mawakili wakujitegemea wanaosimamia kesi
hiyo kutokana na sintofahamu iliyotokea Februari 25 baada ya kesi hiyo
kutotajwa.
Watuhumiwa wote 12 hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama
hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kurudishwa rumande
hadi Machi 27 mwaka huu kesi itakapotajwa tena.
Comments
Post a Comment