
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limewaua
watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamejipanga
kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.
Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa
Wilaya ya Kimbondo,Louis Bura ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi
na usalama wilaya hiyo amesema jana usiku majira ya saa tatu Askari
polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi, kuwa kuna majambazi
wanataka kuvamia baadhi ya nyumba ndipo walipofika eneo la tukio na
kuanza kurushiana risasi na majambazi hao.
Katika tukio hilo askari mmoja
aliyefahamika kwa jina la James Mwita (37) na mama mmoja Sophia Dickson
(60) walijeruhiwa na sasa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya
Kibondo.
Bura amesema askari huyo alipatiwa
matibabu ya awali na sasa hali yake sio mbaya na amepatiwa rufaa kwa
ajili ya kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kwa kuwa amejeruhika sana
mguuni.
Amewapongeza wananchi kwa kuendelea
kuonyesha ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama pia Jeshi la
polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwa ni kazi ngumu na kwamba
wananchi wataendelea kutoa ushirikiano kwa kuwa polisi wako kazini.
Ametoa rai kwa wote wanaojihusisha na
matukio ya ujambazi kuacha mara moja kwa kuwa serikali haitasita
kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na matukio hayo.
Aidha amewataka wananchi kuacha
kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo baadhi wanawakamata
wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na kudai sio
majambazi.
"Niwaambie tu wananchi hatutavumilia
kuona majambazi wanaendelea kututesa Kibondo tumechoka, na kuanzia sasa
niwaombe wananchi wale wanaoshirikiana na raia wa Burundi kuvamia watu
muache maana jambazi hawezi kuja bila kupewa taarifa na watu ambao
wanafahamu ni nani ana pesa, niseme tu kwa sasa tumejipanga tumechoka
haya mambo hatuta wavumilia", alisema Bura.
Aidha amewataka wananchi kuacha kutoka
nje pindi wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya usalama wao kwa kuwa
ni hatari sana kufuata milio hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Wilaya ya
Kibondo Sebasitiani Pima amesema walipokea watu watatu wakiwa wamefariki
naa majeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika
hospitali ya wilaya ya Kibondo na mmoja wamemsafirisha kuelekea Kigoma
kwa ajili ya matibabu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
Wilaya ya Kibondo Khamisi Tahilo ameipongeza serikali na polisi kwa
kazi wanayoifanya na kwamba wananchi wamefurahi sana kwa kuwa
wameshuhudia wenyewe kwa macho yao jambazi mmoja ambaye wamekuta amefia
katika mfereji wa maji wa soko la Mjini na wametoa kiasi cha shilingi
laki moja kuwapa pole askari hao.
Amesema matendo yaliyokuwa yakifanya na
majambazi hao Wilayani humo yamewachosha na sasa wanafuraha sana kwa
kuwa Serikali imeimarisha usalama na ikitokea tatizo lolote
wanawakamata.
Kwa upande wake mmiliki wa nyumba
ambayo majambazi walikuwa wamepanga kuvamia Hamis Salumu amesema
alipigiwa simu na kuambiwa kwamba nyumbani kwake kuna watu wanapiga
risasi ndipo alipokwenda polisi na kukuta tayari polisi walishakwenda
nyumbani kwake.
Amesema
hakuna aliyejeruhiwa wala kilichoibiwa nyumbani kwake na ametoa pongezi
kwa jeshi la polisi kwa ushirikiano wanaouonyesha na kuwataka wengine
wanaojihusisha na shughuli za ujambazi kuacha mara moja kwani mwisho wao
ni mbaya.
Comments
Post a Comment