
Uongozi wa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa North Mara umezungumza
na Serikali kuelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa kudhibiti maji
yenye sumu ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Waziri wa Madini Doto
Biteko, atangaze kufunga shuguli za mgodi huo endapo utashindwa
kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi ya watu, ifike Machi
30 mwaka huu.
Tamko hilo la serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za
haraka za kudhibiti maji hayo ili kukwepa rungu la serikali la kuufunga
mgodi huo. Machi 12, uongozi wa Acacia North Mara ulikutana na Waziri
Biteko ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua
iliyofikiwa ya kutekeleza agizo la serikali.
Uongozi wa kampuni hiyo ukizungumza katika kikao hicho, ulieleza
kuwa, tayari mgodi huo umechukua hatua za haraka tangu kutolewa kwa
agizo na kwamba hadi sasa suala la kudhibiti maji yenye sumu
limeshetekelezwa na hakuna maji yanayotiririka kuelekea kwenye makazi ya
watu.
Aidha, ulimweleza kuwa, pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa
la kuhifadhia maji yenye sumu yajulikanayo kitaalam kama “topesumu”
(Tailings Storage Facility- TSF) mgodi umeanza kuchukuwa hatua za
kujenga TSF mpya.
“Mhe. Waziri tumekuja kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako,
tunafurahi kukuambia kuwa tumetekeleza agizo hilo na kwa sasa hakuna
maji yanayotiririka. Pamoja na hatua hiyo mgodi umeanza mchakato wa
ujenzi wa bwawa jipya (TSF) la kuhifadhia topesumu,” walieleza.
Aidha, ulimweleza Waziri Biteko kuhusu hujuma za uharibifu wa
miundombinu ya bomba la maji yenye sumu unaofanywa kwa maksudi na wakazi
wanaozunguka mgodi ili kufifisha juhudi zao za kudhibiti maji hayo
wakiwa na lengo la kuufanya mgodi uonekane haujachukuwa hatua kudhibiti
jambo hilo, ambapo walionesha picha mbalimbali ya namna bomba lilivyo
pasuliwa ili maji yatiririke kuelekeka kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko alieleza kuwa, amepokea
taarifa ya kampuni husika na kuwapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na
kusema kuwa, ukweli wa jambo hilo atauthibitisha mara baada ya kupata
ripoti ya wataalam watakaokwenda kuhakikisha kuhusu utekelezaji wa agizo
hilo na kuongeza,“katika hili sitanii juu ya kuufunga mgodi ikiwa
utashindwa kudhibiti tope sumu,”.
“Naomba nirudie tena katika hili sitanii, sitabadilisha msimamo wangu
kama serikali na utaendelea kubaki pale pale dawa pekee ni kutekelezwa
kwa agizo hilo. Lakini niseme ukweli, nasikitishwa sana na kitendo hiki
cha wananchi kupasua bomba, kwa hili sikubaliani nao na siwaungi mkono.
Pia, aliongeza kuwa, atawasiliana na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya
kuona namna ya kudhibiti hali hiyo ili wale watakao bainika wachukuliwe
hatua.
Waziri Biteko alilitoa agizo hilo Machi 6, alipoutembelea mgodi huo
hapo kwa ziara ya kikazi pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime.
Comments
Post a Comment