Mambo ya msingi ya kuzingatia ili kufanya biashara yenye faida

Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wengi wanakutana nayo ni kushindwa kujua biashara gani wafanye kwenye maeneo yao ili kuweza kupata faida. Mara nyingi watu wamekuwa wakiomba ushauri sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mitandao kuhusu biashara gani wafanye kwenye maeneo yao.

Ili kuweza kutengeneza biashara yenye faida katika eneo unaloishi au unalopendelea kufanya biashara yako nakushauri ufanye mambo haya matano.

1. Fanya utafiti mdogo wa kujua biashara gani inayofaa kwa eneo hilo.
Ni muhimu sana kufanya utafiti mfupi ili kujua kama wazo lako la biashara linaweza kufanikiwa kwa eneo unalotaka kufanyia biashara. Sio kila wazo la biashara linaweza kutengeneza biashara kubwa na yenye faida.

2. Kuwa tofauti, kuwa mbunifu.
Kama kuna soko la biashara unayotaka kufanya ni dhahiri kwamba kuna watu wengine wanafanya biashara hiyo. Jiulize ni jinsi gani unaweza kujitofautisha na watu hao? Kama huna njia ya kujitofautisha nakushauri tu uachane na hiyo biashara maana utaumiza sana kichwa. Hakuna kitu kinachoumiza kichwa kwenye biashara kama ushindani usiokuwa na tofauti, kama kuna mwenye mtaji mkubwa kushinda wewe atakuondoa sokoni. Mara zote jua ni mbinu gani za kibunifu na za utofauti za kukuwezesha kukuza biashara yako.

3. Kua kwanza wewe ndio biashara yako ikue.
Inashangaza ni kiasi gani watu wanataka biashara zao zikue wakati wao wenyewe hawakui. Jua siri hii moja ”Lazima wewe ukue kwanza ndipo biashara yako nayo ikue”. Ili wewe kukua unahitaji kujifunza kila siku kuhusiana na biashara unayofanya na biashara nyingine kwa ujumla. Tunaishi kwenye zama ambazo kujifunza kuko kwenye ncha za vidole, mtandao una kila kitu unachotaka kujifunza. Tembelea mitandao ya kujifunza na utapata mbinu bora ka kukuza biashara yako. Usitegemee kufanikiwa kwa kufanya biashara kwa mazoea, kujifunza ni muhimu sana.

4. Kuwa na usimamizi wa kutosha kwenye biashara yako.
Watu hawaaminiki kwenye fedha, ni tatizo sana kama umejinyima na kupata mtaji wa biashara halafu unaianzisha na kuwapa watu wengine waisimamie. Ni rahisi sana kushindwa au kupata hasara kwa njia hii. Ni vigumu sana kupata mtu anayeweza kuwa na uchungu na biashara yako. Nakushauri kama huna muda wa kufuatilia biashara yako kwa karibu ni heri utumie hiyo fedha yako kufanya mambo mengine yatakayokuingizia fedha kidogo kuliko kwenda kuipoteza huku ukiona.

5. Kuwa na uvumilivu.
Kama kila ukianzisha biashara na kuona hailipi unaacha na kuanzisha nyingine, utafanya kila aina ya biashara na hutaona mafanikio yoyote. Bishara sio rahisi kama watu wanavyoamini, biashara inahitaji uvumilivu na ustahimilivu. Ni vigumu na mara chache sana mtu anaweza kuanzisha biashara na akaenda vizuri bila ya kupata misukosuko. Kwenye biashara halisi kuna misukosuko mingi sana, unaweka mkakati mzuri na kujua faida itapatikana ila vinatokea vikwazo na kukurudisha nyuma. Katika nyakati hizi ndio unatakiwa kujifunza na kama ukivuka nyakati ngumu unakuwa umeongeza kinga kwenye biashara yako. Unapojifunza utajua ni wapi ulipokosea hivyo kuepuka kurudia makosa.

6. Usiitegemee biashara mwanzoni.
Kama nilivyosema hapo juu biashara inachukua mwaka mmoja na wakati mwingine miaka miwili kuweza kusimama na kujiendesha yenyewe na kutengeneza faida. Kipindi cha mwanzo cha biashara ni kigumu sana na hutakiwi kuondoa fedha yoyote kwenye biashara kwa matumizi yasiyo ya biashara. Usianzishe biashara na wakati huo huo ukaanza kuitegemea kwa kuishi, biashara hiyo itakufa.

Biashara ni nzuri sana kama umejipanga na unajua ni nini unafanya. Ila kama hujajipanga au umeiga, biashara inaweza kuwa ngumu sana kwako kiasi cha kuachana nayo kabisa. Kwa ushauri huu nafikiri unaweza kubadili mtazamo wako na mbinu za kufanya biashara.

Comments