Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ushirika na
Umwagiliaji Joseph Machibya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe
Wilaya ya Bukombe amemuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha anaweka
kipaumbele ununuzi wa dawa hasa za vitamin A kwa ajili ya kuboresha
afya za watoto chini ya umri wa miaka mitano katika ukuaji wao.
Wito huo ameutoa katika kikao cha
mapitio ya shughuli za lishe kwa kipindi cha Julai – Disemba 2018
katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauli tarehe 5 Februari, 2019.
Pia Machibya amemuagiza Afisa Lishe
Wilaya kuhakikisha anawashirikisha wadau wote katika uandaaji wa bajeti
2019/2020 ili Halmashauri iwe na mpango mkakati mmoja utakao leta tija
katika suala la lishe bora.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za lishe Julai –Disemba 2018 Afisa Lishe Wilaya Ladislaus
Willium Magaso alisema hadi kufikia Disemba 2018 IMA world Heaith ilitoa
Tsh. 57,601,000/= kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe ambazo
ni ufuatiliaji wa matumizi ya chumvi yenye madini joto, ukaguzi wa
wafanyabiashara wa chumvi, kutembelea kaya zenye watoto chini ya umri wa
miaka mitano ili kutoa elimu ya lishe bora, kufanya mikutano kwa
wasimamizi wa wahudumu wa afya ngazi ya kijiji, kufanya mikutano ya
kamati ya uendeshaji wa shughuli za lishe ngazi ya Wilaya, uhamasishaji
juu ya ulishaji sahihi wa watoto, kuwezesha wajumbe wa kamati ya Afya
ya Wilaya kukusanya takwimu na ufuatiliaji wa zoezi la utoaji wa
Vitamini A na dawa za Minyoo.
Kwa upande wake Katibu wa Afya Wilaya ya
Bukombe Zacharia Isack alisema hapo nyuma kulikuwa na changamoto ya
uchangiaji wa huduma za afya uliopelekea mapato ya huduma za afya
kushuka, baada kuanzishwa kwa mfuko wa afya ya jamii (CHF iliyoboreshwa)
tunategemea kuwepo kwa ongezeka kubwa la mapato ya ndani
yatakayopelekea kuboresha maisha ya akinamama wajawazito na watoto chini
ya umri wa miaka mitano kwa asilimia kubwa.
Mkuu wa Idara ya Kilimo,
Ushirika na Umwagiliaji Joseph Machibya akifungua kikao kwa niaba
Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Wilaya ya Bukombe
Afisa Lishe Wilaya Ladislaus Willium Magaso akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe
Mwekahazina wa Wilaya ya Bukombe John Bernard Majubu akichangia mada wakati wa kikao
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya lishe Wilaya
Comments
Post a Comment