Naibu
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.
Faustine Ndugulile amewaagiza watendaji wa halmashauri zote nchini
kutotumia wakandarasi kujenga miradi mbalimbali inayohusu sekta ya afya.
Ametoa
agizo hilo mkoani Ruvuma wakati alipotembelea na kujionea ukarabati na
ujenzi wa Chuo cha Wauguzi Songea na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale
katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Amesema kuwa miradi hiyo inatakiwa kutumia mtindo wa 'Force Account', ambao unatumia mafundi wa kawaida kujenga miradi hiyo.
"Fedha
zote za maendeleo Ndani ya Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, utaratibu utakuwa ni 'Force Account'. Kibali
cha kwenda kwa wakandarasi kitatoka kwa mawaziri, kwasababu mwisho wa
siku ninayewajibika ni mimi", amesema Dkt. Faustine Ndugulile.
Naibu
Waziri Ndugulile amefikia hatua hiyo baada ya kupokea taarifa ya kuanza
kwa mchakato wa ujenzi wa baadhi ya majengo na ukuta wa Chuo cha
Waganga mkoani humo, ambao ungegharimu zaidi ya shilingi milioni 900,
akisema kwamba endapo ungetumika mfumo wa 'Force Account' zingejenga
jengo hilo na ukuta.
Chanzo:Eatv
Comments
Post a Comment