Watoto 10 wenye umri kati ya miaka miwili hadi sita wamechinjwa na
kukatwa koromeo, sehemu za siri, masikio na ulimi wilayani Njombe mwezi
huu.
Kutokana na matukio hayo yanayodaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina,
mkuu wa wilaya hiyo, Ruth Msafiri ametoa amri kwa wazazi na walezi
kuwapeleka na kuwafuata shule watoto wao. Pia, ameagiza watoto wote
wilayani humo kuhakikisha kuwa wanatembelea kwa makundi.
Aidha, mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema, “Imani
za ushirikina na malipizo ya visasi ndivyo vinaleta haya mambo,
nimeagiza vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi kupitia upya
leseni za waganga wote wa jadi na kuwakamata wale wote wanaohusishwa
kutoa maelekezo yanayosababisha vifo vya watoto na watu wazima kwa imani
za kishirikina.”
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema taarifa
alizonazo ni za matukio mawili ambayo polisi wanayafanyia kazi.
Lakini wakati Lugola akisema hayo, Msafiri alisema mtoto wa 10 aliokotwa
jana akiwa amechinjwa na kunyofolewa viungo. Alisema watoto sita
wamefanyiwa ukatili huo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na wanne
wanatoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
“(Kati ya) sita waliookotwa (wakiwa wamekufa) Halmashauri ya mji
Njombe, wawili walipotea na kuokotwa wakiwa wameuawa misituni, wawili
wameokotwa maeneo tofauti wakiwa wamekufa na hawakutambulika, wamezikwa
na halmashauri,” alisema.
Comments
Post a Comment