Uchaguzi DRC: Martin Fayulu apinga matokeo ya urais DRC, Felix Tshisekedi afurahia na kumtaja Kabila kuwa 'mshirika muhimu'
Martin Fayulu, mgombea urais wa upinzani DRC aliyeibuka wa pili, ameyakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Matokeo
ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) yanaonesha
Felix Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na
"anatangazwa mshindi mteule wa urais."Bw Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akimaliza wa tatu akiwa na takriban kura 4.4 milioni.
- Upinzani DRC: Fayulu asema matokeo ya uchaguzi hayana mjadala
- Mgombea mkuu wa upinzani DRC Martin Fayulu ni nani?
- Makundi mawili ya upinzani yaliyoibuka uchaguzi DRC
Ameendelea: "Bw Nangaa (mwenyekiti wa CENI) anafuma kitambaa cheusi kwa uzi wa rangi nyeupe. Natoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo yao.
Bw Nangaa na marafiki zake katika FCC [chama tawala] wamekuwa wakichakachua matokeo kumpa 'kikaragosi' wao ushindi."
Awali, alikuwa ameambia kituo cha redio ya Radio France International (RFI) kwamba matokeo hayo ni "mapinduzi halisi kupitia uchaguzi" na akatoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo waliyo nayo aliyosema ni ya kweli.
Nchini DRC hata hivyo, ni kinyume cha sheria kwa mtu mwingine kando na CENI kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Mshindi mteule wa uchaguzi huo uliofanyika 30 Desemba mwaka jana, Bw Tshisekedi, kwa upande wake ameyafurahia matokeo hayo na kumsifu pia rais anayeondoka Joseph Kabila.
Amemweleza kama "mshirika muhimu kisiasa."
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mji mkuu Kinshasa, Tshisekedi amesema atakuwa "rais wa raia wote wa Congo".
Kumekuwa na tetesi kwamba kucheleweshwa kwa shughuli ya kutangaza matokeo, ambayo awali yalitarajiwa kutangazwa Jumapili, kulitoa muda kwa Rais Kabila na Bw Tshisekedi kuafikiana.
Matokeo yaliyotangazwa na CENI:
- Felix Tshisekedi 7,051,013 (38.57%)
- Martin Fayulu Madidi 6,366,732 (34.83%)
- Emmanuel Shadary 4,357,359 (23.84%)
Kanisa Katoliki limesema matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume hiyo yanakinzana na matokeo ambayo yameandaliwa na waangalizi wake.
Wamedokeza kwamba Bw Fayulu alipata kura nyingi, kwa mujibu wa takwimu walizo nazo. Baadhi ya kura za maoni zilikuwa zinamuonesha Bw Fayulu akiwa mbele ya wagombea wengine.
Msemaji wa Bw Tshisekedi Claude Lbalanky ambaye amesema siku ya leo ni "siku njema kwa taifa" ameambia BBC kwamba hakuna makubaliano yoyote kati ya Rais Kabila na Bw Tshisekedi.
"Tuna furaha sana, sana sana. Hii ni siku njema kwa DRC. Mnafahamu kwamba maoni ya wananchi yameheshimiwa. Kwa hivyo, tumefurahia sana."
Kuhusu makubaliano, amesema: "Hilo si kweli hata kidogo. Ukweli ni kwamba hauwezi kuwa na kukabidhiana mamlaka bila vyama kuzungumza. Ilipobainika wazi kwamba tungekuwa washindi, tulikwenda kumuona rais anayeondoka Rais Kabila na kuona jinsi shughuli ya mpito inaweza kufanywa kuwa laini. Sawa.
"Tumeshuhudia jambo kama hilo likitokea Afrika Kusini pale (Nelson) Mandela alipochukua mamlaka kutoka kwa utawala fidhuli wa ubaguzi wa rangi. Ni lazima kuwe na mazungumzo ya aina fulani, kusema 'ehee, nyinyi mmeshinda. Nitakuwa salama?'. Kwa hivyo, bila shaka hakukuwa na zaidi ha hayo. Kwa hivyo, hakukuwa na makubaliano yaliyoathiri matokeo yauchaguzi."
Ushindi wa kihistoria
Mwandishi wa BBC Louise Dewast anasema ushindi huo uliotangazwa na CENI ni wa kihistoria kwa chama cha UDPS na Tshisekedi mwenyewe.Chama hicho cha upinzani kimejaribu kwa miaka mingi kushinda uchaguzi DRC bila mafanikio. Lakini katika siku za karibuni kumekuwa na tetesi kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mwafaka kati ya Tshisekedi na rais Joseph Kabila hatua ambayo ilizua wasiwasi miongoni mwa wanasiasa wa upinzani.
Bw Tshisekedi mwenyewe amekiri kwamba alifanya mazungumzo na chama tawala lakini kuhusu maandalizi ya kipindi cha mpito.
Swali kuu kwa sasa ni jinsi wananchi na wadau wa kisiasa watayapokea matangazo hayo. Kanisa Katoliki ambalo lina waumini wengi na lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi maeneo mengi lilikuwa limetahadharisha kwamba litayakataa matokeo iwapo hayatakuwa ya kweli. Kanisa hilo lilikuwa limesema linamfahamu mshindi wa urais na kwamba alikuwa ni mshindi wa wazi.
Martin Fayulu ni nani?
Mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Martin Fayulu ni miongoni mwa watu wenye ushawishi katika siasa nchini.Ni mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 61.
Majengo ya tume ya uchaguzi DRC yateketea
Wasifu wa mshindi wa urais DRC Felix Tshisekedi
Martin mbali ya kujihusisha na masuala ya kisiasa ni mfanya biashara maarufu nchini Congo, miongoni mwa vitega uchumi vyake ni umiliki wa hoteli.
Alisomea nchini Marekani, Ufaransa lakini pia aliwahi kufanya kazi katika makampuni makubwa ya simu nchini Marekani.
Alikuwa mstari wa mbele katika kumfanyia kampeni ya kisiasa aliyekuwa kiongozi wa upinzani marehemu Ettiene Tshisekedi.
Aliwahi kukamtwa mara kadhaa katika maandamano ya upinzani nchini.
Wengi walishangazwa na kuchaguliwa kwa Fayulu kando na kwamba ni mbunge, wengi wanamtazama kama mfanyabiashara kuliko kiongozi wa upinzani.
Comments
Post a Comment