NAIBU WAZIRI WA MADINI AWAHAMASISHA WACHIMBAJI WADOGO KUFANYA UCHIMBAJI WENYE TIJA



Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko amewashukia wachimbaji wadogo wadogo wa Kata ya Katente Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita,akiwataka kufanya kazi ya uchimbaji wa dhahabu kwa kufanya utafiti akinifu  ili wainuke kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa kulipa kodi.
 
Biteko aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili ya wachimbaji wadogo wadogo katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ili watambue umuhimu wa utafiti na manufaa watakayo yapata kupitia mradi mkubwa wa kuchenjua dhahabu unaojengwa maeneo ya Katente.
Alisema serikali imetenga fedha za kigeni Dola 3.7 milioni sawa na Tsh Bilioni 8.5 za kitanzania kwa ajili ya kufanyia utafiti wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo wadogo Wilayani hapa, ili waachane na uchimbaji wa kubuni na kutumia waganga wa kienyeji kufanya utafiti kwa kupigiwa ramri huku wakilazimikia kuhama hama na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa kuacha mashimo na kukata miti.
 
Mkurugenzi wa jiolojia na utafiti Tanzania Mavuruko Msechu alisema utafiti wa madini Kata ya Katente ulianza Agost 2016 kutokana na kubaini kuna dhahabu serikali imetega fedha ambazo zitajenga mradi wa kuchenjua dhahabu utakao wanufaisha wananchi.
Msechu aliongeza kuwa serikali imetuma watalam ili kufanya utafiti wakuleta tija kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Mwenyekiti wa wachimbaji Madini Mkoa wa Geita Chiristoper Kadeo  alisema wachimbaji awali walikuwa wakichimba kwa hali duni na tafiti kunyanyika kwa kutumia waganga wa kienyeji kwa kupitia kuchana kuku ili aoneshe miamba ya dhahabu ilipo.
Kadeo alisema mafunzo haya yatawapa mwanga wakuto tegemea waganga wa kienyeji katika kuchimba dhahabu kutokana na serikali kuwapa mafunzo na kuleta watafiti hali hiyo itawafanya kuondokana na tafiti duni.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika kwa wachimbaji wa dhahabu Katente Paul Mapigi alisema mradi huo wa kuchenjua dhahabu wameupokea na kwamba utarahisisha uchimbaji na kunusuru wananchi kuendelea kuathiriwa na sumu ya Zekabi.

Comments