Matokeo ya Uchaguzi wa Urais DRC huenda yakachelewa


Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasema matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu huenda yakachelewa na kupita tarehe iliyotarajiwa ya Januari 6.

Rais wa tume hiyo, Corneille Nangaa, amesema kituo kikuu cha kuhesabia kura bado kinasubiri matokeo ya zaidi ya asilimia 80 ya kura zilizopigwa kutoka vituo mbalimbali kote nchini humo.

Aidha amesema bado ni mapema mno kubaini chanzo cha kuchelewa kwa matokeo hayo, lakini vyama vya upinzani vinadai hiyo ni njama ya kuiba kura.

Wakati huo huo shirika la Umoja wa Afrika pamoja na Shirika la Kimaendeleo la Kusini mwa Afrika - SADC yametaja uchaguzi huo kama ulioendeshwa vizuri kwa kiwango kikubwa, licha ya kuwa na matatizo kadhaa ya kiufundi pamoja na machafuko katika baadhi ya maeneo.

Waangalizi pia wamesema baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kuchelewa na kusababisha kucheleweshwa kwa zoezi hilo.

Wameongezea kuwa wapiga kura hawakuelimishwa vizuri kuhusu utumizi wa vifaa vya kielektroniki vya kupigia kura ambavyo vimetumika kwa mara ya kwanza nchini humo

Comments