Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe yaanzisha madarasa lishe


 
Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kupitia shirika la IMA World Health inatekeleza mpango wa mabadiliko chanya ya  afya  na lishe kuanzia watoto wenye umri chini ya miaka 5  kwa kuanzisha  madarasa lishe katika  kata ya Bugelenga vijiji vya Bufanka, Bugelenga, Mkange na Msasani lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wote wanapata uzito unaostahili kulingana na umri wao ili kupata jamii yenye watoto  werevu.
Hayo aliyasema Afisa lishe wa Wilaya ya Bukombe Ndg. Ladislaus Willium Magaso  wakati akitoa taarifa ya upimaji wa watoto katika kikao cha kamati ya lishe ya Wilaya kilichofanyika  tarehe 19 Januari, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.

Ladislaus alisema mpango wa Halmashauri ni kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinaanzisha madarasa lishe kwa ajili ya kupunguza changamoto inayowakabili watoto chini ya umri wa miaka 5 kwa kuwa mpaka sasa jumla ya watoto 227 katika kata ya Bugelenga waliopimwa uzito kati yao watoto 113 wanalishe bora na watoto 114 wanautapiamlo (unauzito pungufu kulingana na umri wao).

Pia amewaomba mafisa elimu Msingi na Sekondari kuhakikisha wanawasisitiza wakuu wa shule pamoja na walimu wakuu kuanzisha mpango wa chakula shuleni  ili  wanafunzi waweze kupata chakula bora wakiwa shuleni.

Akichangia taarifa ya kampeni ya utoji wa vitamin A katika kikao hicho Mratibu wa chanjo Wilaya Ndg Simon Misusi alisema kupitia mpango wa kumfikia kila mtoto kwa chanjo wameweza kuhamasisha vituo kumi ambavyo ni hospitali ya Wilaya ya Bukombe, kitu cha Afya Uyovu, Ikuzi, Ushirombo, Iyogelo, Bugelenga, Mienze, Bukombe pamoja na Bugando na kuhakikisha watoto wote kuanzia miezi 6 hadi miezi 59 wanapata  vidonge vya vitamin A pamoja na dawa za minyoo.

Akihitimisha kikao hicho  Mkuu wa Idara ya Kilimo Ndg. Joseph Machibya kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji aliwaomba wajumbe kuhakikisha  wanaweka shughuli za lishe kwenye bajeti ya  mwaka wa fedha 2019/2020 ili kupata  watoto wenye afya njema ambao watakuwa viongozi kwa siku za baadaye.


Comments