Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
imesema joto limeongezeka kutoka nyuzi joto 31 hadi 35 katika ukanda wa
pwani kwenye mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Tanga na Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari leo Desemba 3,
2018 jijini Dar es salaam, Meneja wa Kituo Kikuu cha utabiri cha
mamlaka hiyo, Samuel Mbuya amesema ongezeko la joto katika ukanda huo
limetokana na mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli na kuwepo kwa jua la
utosi.
Mbuya amesema hali hiyo inatarajiwa
kuisha Januari, 2019 lakini itarejea tena Februari, 2019 kwa sababu
kutakuwa na jua la utosi.
"Joto limeongezeka kutokana na mwenendo
wa kawaida wa jua la utosi na mtawanyiko hafifu wa mvua za vuli. Mvua
zinaponyesha huwa zinapoza joto, tunatarajia hali hii itakwenda mpaka
Januari," amesema Mbuya.
Watalaamu wa masuala ya afya wanasema
joto linapoongezeka huchangia kudhoofisha nguvu ya mwili katika utendaji
wa kazi, hususan pale mtu anapokuwa sehemu ya wazi, wanasema, mara kwa
mara mtu anapaswa kunywa maji mengi ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha
ufanisi wa mifumo katika mwili wa binadamu.
Chanzo - EATV
Comments
Post a Comment