
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Jeshi la Polisi lipo
imara kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza nchini hivyo
wahalifu wasithubutu kulichezea, wala ‘kulibipu’.
Lugola
pia amewataka wananchi kuendelea kuwapa taarifa za uhalifu Polisi ili
ziweze kufanyiwa kazi haraka kwa kuwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli
si ya kuchezewa na imejipanga kikamilifu kwa kuwalinda wananchi wake.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Ragati, Kata ya
Kasuguti, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, Lugola alisema
Jeshi la Polisi lipo imara na litaendelea kuwalinda wananchi pamoja na
mali zao, ila Polisi ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi,
wananchi wanapaswa kuwasaidia katika kufichua uhalifu katika maeneo yao
wanayoishi.
Lugola
aliyazungumza hayo baada ya wananchi wa Kijiji hicho kumlalamikia kuwa
kuna kundi la vijana ambalo linaongozwa mwananchi mmoja kijijini hapo
wanahatarisha amani na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi na kushindwa
kufanya shughuli zao za maendeleo.
“Polisi
wapo kwa ajili yenu hivyo kuweni huru muda wowote kutoa taarifa za
kiuhalifu katika maeneo yenu, hivyo kutokana na viashiria hivyo vya
uvunjifu wa amani katika Kata hii namuagiza mkuu wa polisi wilaya (OCD)
kuwasaka, kuwakamata wale wote ambao wanahatarisha amani katika Kata hii
ya Kasuguti,” alisema Lugola. Lugola aliongeza kuwa, yeye ni Mbunge wa
Jimbo hilo na pia ni Waziri ambaye anasimamia usalama wa wananchi na
mali zao, hivyo hatakubali wananchi waishi kwa wasiwasi katika maeneo
yao na nchi kwa ujumla, na pia Serikali ya Magufuli haichezewi,
haijaribiwi na wala haibipiwi na mtu yeyote.
Amesema
licha ya polisi usiku na mchana wanalinda wananchi na mali zao lakini
pia wananchi ni wadau wakubwa kwasababu wana mengi wanayaona mitaani
kwao hivyo kwa baadhi ya wale wenye tabia ya kuficha matukio ya uhalifu
ni hatari kwa usalama wao. Aidha, Lugola aliwataka wananchi wa Kata hiyo
waendelee kufanya shughuli za kimaendeleo katika vijiji vyao na pia
waanze maandalizi ya kilimo, naye atahakikisha anatoa misaada mbalimbali
ikiwemo mbegu ili wananchi hao waweze kupata mazao yaliyo bora kwa hapo
baadaye.
Lugola
pia alijibu maswali mbalimbali ya wananchi hao, yakiwemo kuhusu
maendeleo ya Jimbo lao na pia kuhusu Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa kuhusu kuwapa vitambulisho. Hata hivyo, kwa
upande wa wananchi kupata vitambulisho vya taifa, Lugola aliendelea
kusisitiza kuwa, Vitambulisho hivyo vitatolewa kwa watanzania wenye sifa
na haki yao kupata lakini ili waweze kupata vitambulisho hivyo lazima
wapitie katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wasio raia.
Amesema
mchujo huo unaofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) upo
makini ili kuhakikisha hakuna makosa yatakayofanywa wakati wa utoaji wa
vitambulisho, hivyo wananchi wawe na uvumilivu wakati mchujo huo
ukiendelea. Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake akisikiliza kero za
wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi,
mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao
hayo kwa wingi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara,
Kangi Lugola (kulia), akimsindikiza kumpeleka ndani ya gari Mkazi wa
Kitongoji cha Songambele, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara mwenye umri
wa miaka 100, Mzee Mtatiro Silla, mara baada ya Waziri huyo kumaliza
mkutano wake wa hadhara akizungumza na wananchi wa Kata hiyo, Wilaya ya
Bunda, Mkoani Mara, leo.
Lugola
aliwataka wananchi jimboni kwake watoe polisi taarifa za uhalifu nchini
na pia Serikali ya Awamu ya tano ipo imara haichezewi na mtu yeyote.
Pia Lugola aliwataka wananchi jimboni kwake waanze maandalizi ya kilimo.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Comments
Post a Comment