
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homela.
Zaidi
ya watu 20 wanaojihusisha kununua korosho kwa utaratibu usio rasmi kwa
wakulima, maarufu kama kangomba wamekamatwa wilayani hapa akiwemo diwani
wa Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
Juma Homera, alisema watu 14 tayari wamefikishwa mahakamani na wengine
akiwemo diwani huyo wanaendelea kushikiliwa na polisi.
“Wananchi
walitutumia sms (ujumbe mfupi wa simu) na tulitumia pia vyanzo vyetu
vingine vilivyoko vijijini kubaini kangomba,” alisema Homera.
Alisema walimkamata mtu mmoja aliyekutwa akibadilishana na wakulima kwa kuwapa kilo moja ya nyama kwa kilo tatu za korosho.
“Huyo mtu alikutwa nyumbani katika Kijiji cha Nangorembe akiwa amechinja ng’ombe wanne, anagawa nyama kwa wananchi,” alisema.
Homera
alisema pia katika Kijiji cha Kitanda walikamata watu saba waliokutwa
na tani saba za korosho zenye thamani ya Sh milioni 75.
Alisema watu hao walikamatwa katika vijiji vya Mneche, Tinginya, Namiungo, Majimaji na Kitanda.
Kuhusu
Diwani wa Kata ya Nalasi Magharibi, Khalifa Kabango (CUF), alisema
alikamatwa juzi katika operesheni iliyofanywa Tarafa ya Nalasi ambako
vilikamatwa viroba vya korosho 31 vikiwemo vya diwani huyo.
Alisema
diwani huyo bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Tunduru na
kwamba alikuwa akinunua korosho kwa bei ya Sh 1,500 kwa kilo ili apeleke
vyama vya msingi akapate fedha zaidi.
“Baadhi
ya matajiri wamekuwa wakituma fedha vijijini na wenyeji ndio wanaonunua
korosho hizo halafu wakikamatwa ndio wanawataja mabosi waliowatumia,”
alisema.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema pia baadhi ya makarani wa vyama vya msingi
wamekuwa wakitumia mawe ya mzani yaliyochezewa na kuwapunja wakulima.
Kwa
mujibu wa DC huyo, mawe yaliyochezewa ni ya kilo 50 na kwamba katika
kila jiwe la aina hiyo mkulima anaibiwa wastani wa kilo 5.5 hadi 6.
Alisema wamemkamata karani wa chama cha msingi, Mohamed Msamati kwa madai kuwa alikuwa akiwaibia wananchi kilo 5.5.
Kuhusu wakulima waliolipwa alisema hadi sasa wamelipwa 534 na Sh milioni 550.7 zimetumika.
“Tukimtilia
mtu shaka kama kilo zake zimezidi tunakwenda kuangalia shamba lake
kwanza halafu tunalinganisha na kilo alizopata mwaka jana,” alisema
Homera.
Alisema
hadi sasa zaidi ya tani 5,000 zimeshakusanywa katika maghala na
zinaendelea kusafirishwa kupelekwa katika ghala kuu Mtwara kwa usimamizi
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Hadi
sasa tumeshasafirisha tani 166 na kilo 891 na magari matano ya JWTZ
yameshaondoka na mengine matano yanaendelea kupakiwa,” alisema.
Homera
alisema bado wanaendelea na kazi ya uhakiki wa majina ya wakuliwa
wanaostahili kulipwa na kama kuna udanganyifu hatua za kisheria
zitachukuliwa kwa wahusika.
Hata
hivyo juzi wakati uhakiki wa majina ya wakulima wa korosho ukiendelea
mkoani Mtwara, iliripotiwa kuibuka kwa majina hewa, likiwamo la mwenza
wa karani wa chama cha msingi.
Katika
uhakiki huo ambao unafanyika usiku na mchana kwa ajili ya malipo ya
wakulima, yamebainika majina matatu katika Chama cha Msingi cha Makonga
wilayani Newala.
Akizungumzia
hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo, alisema
walibaini majina hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisema mmoja wa makarani wa Makonga (jina linahifadhiwa), aliandika malipo hewa kwa jina la mpenzi wake (jina linahifadhiwa).
“Kutokana na uhusiano wao wa mapenzi, ameamua kumwandikia malipo hewa na kuna wengine wameandika ndugu zao.
“Tumekamata kilo 200 ambazo zimeandikwa malipo hewa, kama hali ndiyo hii kwa makarani wengine ikoje?
“Tunawaomba
wananchi waendelee kutoa ushirikiano, wajumbe wa bodi, wenyeviti na
makatibu wa Amcos zote wawe makini na waandike kile ambacho ni sahihi,”
alisema Mangosongo.
Alisema
karani huyo na wote waliohusika kuandika majina hewa wanaendelea
kuhojiwa na utafanyika uhakiki katika kila shamba la mkulima na
kujiridhisha na korosho alizowasilisha.
“Mtu hana shamba lakini unakuta jina lipo na akaunti namba, tukiwagundua wengine tutakula nao sahani moja,” alisema.
Comments
Post a Comment