Yondani Ametenda Dhambi Kama Ya Rijkaard, Apewe Adhabu Kali.


Ndugu zangu, Aliyetaka kuona aliona jana. Kelvin Yondani, tena un-provoked- bila kuchokozwa, alimtemea mate Asante Kwassi. Na katika mechi hiyo hiyo alimpiga kiwiko John Bocco.
Nilishangaa refa hakumpa red card Yondani kwa kumtemea mate Kwassi huku Kwassi akimwonyesha Refa ushahidi wa mate mazito shavuni. Haiwezekani Kwassi kujitemea mate.
Tukio kama la jana lilitokea kwenye robo fainali ya kombe la dunia 1990 pale Rudi Voller na Frank Rijkaard walipochuana vikali. Ikafika mahali wakaanza kujibishana maneno na ndipo Rijkaard akamtemea mate Voller. Refa aliwapiga red wote wawili.
Tofauti ya Rijkaard na Yondani iko wapi?
Rijkaard na Voller wao walikwazana kimchezo na tuliona. Refa aliwapa red wote kwa vile alijua kuwa Rudi Voller alikuwa akim-provoke Frank Rijkaard muda mwingi wa mchezo. Kitendo cha Rijkaard kumtemea mate Rudi ikawa ukomo wa refa kuvumilia ujinga wao. Kwenye soka kumtemea mate mchezaji mwenzako ni kitendo kisicho cha kimpira na hakivumiliki.
Kwanini Yondani apewe adhabu kali?
Ndugu zangu,
Ushahidi upo, tena wa dhahiri. Kuacha kitendo cha utovu wa nidhamu kipite bila muhusika kuadhibiwa ni kukaribisha matendo kama hayo kwenye soka letu. Yanaweza kuwa chanzo cha vurugu uwanjani na nje ya uwanja.
Kamati ya Nidhamu ya TFF bila shaka itapitia yaliyojiri kwenye mechi ya jana na kwamba Kelvin Yondani, tena akiwa Nahodha Msaidizi, anastahili kupewa adhabu kali itakayoipendeza Kamati ya Nidhamu ya TFF isipokuwa kifungo cha kucheza mpira maana ndio ajira yake Kelvin Yondani.
Maggid Mjengwa

Comments