Odinga Awataka Wafuasi Wake Kusitisha Kususia Bidhaa Za kampuni Nne.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amewaambia wafuasi wake wasitishe kampeni ya kususia bidhaa na biashara za kampuni zilizohusishwa kuwa na uhusiano na chama tawala nchini Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta.
Safaricom, kampuni kubwa ya mawasiliano ya simu nchini na Brookside, ambayo ni kampuni ya kutengeneza bidhaa kama maziwa na siagi ni miongoni mwa kampuni zilizolengwa.
Bwana Odinga alitoa tamko hilo leo katika sikuukuu ya Mei mosi katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Kampuni ambazo Muungano wa Upinzani NASA ulisema wafuasi wake wazisusie ni pamoja na:
•Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ambayo ndiyo tajiri zaidi miongoni mwa kampuni za Kenya
•Kampuni ya maziwa ya Brookside, inayomilikiwa na familia ya Kenyatta
•Kampuni ya kutengeneza mafuta ya kupikia na sabuni ya Bidco
•Kampuni ya Haco inatengeneza na kusambaza bidhaa za urembo, na za usafi wa nyumba nchini Kenya, Uganda, na Tanzania
Muungano wa upinzani Nasa uliyaorodhesha makampuni hayo kwa kile ilichokitaja kuunga mkono utawala usio halali uliomnyima Raila ushindi katika uchaguzi mkuu mwaka jana

Comments