WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo
inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe umuhimu wa
elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
“Kwa ujumla utoro wa wanafunzi
wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa Mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie
nafasi hii kuikumbusha Mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi,
walezi na wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumatatu, Aprili 02, 2018) wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa
mwaka 2018 katika uwanja wa Magogo mkoani Geita. Kaulimbiu ya mbio za mwenge
kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya
Taifa letu.’
Waziri Mkuu amesema dhamira ya
Serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali
wa maendeleo kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na
stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa
kati ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu utoro kwa
shule za sekondari nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Tabora ndio unaongoza
kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,
Kuhusu utoro wa wanafunzi wa
shule za Msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni wa Rukwa kwa
asilimia 3.2, Geita asilimia 3.1, Tabora asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na
Singida asilimia1.9.
Amesema mikoa yenye kiwango
kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule ihakikishe mahudhurio
yanadhibitiwa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa
wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu ngazi husika.
“Ukitaka kuleta maendeleo ya
uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya
uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, lazima
uwekeze zaidi katika elimu”
“Kwa hiyo, uwekezaji katika
elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu na Watanzania kwa jumla wanapata
haki yao ya msingi bali ni kuweka misingi imara itakayo liwezesha Taifa na mtu
binafsi kufikia hatua bora ya maisha”.
Waziri Mkuu amesema ili
kuhakikisha Taifa linafikia viwango bora vya elimu, Serikali ya awamu ya tano
inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imedhamilia kuboresha elimu katika
ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitaendelea kuhimiza
mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu bado ipo na inaendelea kuwa ni adui wa
haki na kudhoofisha jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi, kuimarisha huduma
za jamii na Utawala bora.
Amesema athari zinazotokana na
vitendo vya rushwa huwaathiri watu wa kawaida zaidi na kuendelea kubaki
wanyonge katika jamii, hivyo Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya
rushwa bila kuchoka mpaka jamii itakapoachana na vitendo hivyo vya kidhalimu.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bibi Jenista
Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa takribani kilomita
103,440.7 kwa siku 195 katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya
195.
Alisema kazi hiyo itafanywa na
vijana sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao wameandaliwa
kikamilifu ili kuhakikisha wanaendelea kuwakumbusha Watanzania historia ya
falsafa ya Mwenge wa Uhuru, kufikisha kwa ufasaha ujumbe wa mwaka huu na
kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo kwa umakini.
Naye, Waziri wa Vijana,
Utamaduni, Sanaa na Michezo – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ali Abeid
Karume alisema atahakikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unawafikia wananchi wote
pamoja na kupita katika miradi yote ya maendeleo iliyopangwa.
Balozi Karume ametumia fursa
hiyo kuwapongeza Rais Dkt. Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali
Mohammed Shein kwa jitihada zao za kudumisha amani, utulivu, kuwaletea wananchi
maendeleo bila ya ubaguzi pamoja na kupambana na maadui wanaotaka kudhoofisha
maendeleo nchini.
Comments
Post a Comment