
Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini kuhakikisha
wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwa ni pamoja na
kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Kauli hiyo imetolewa Jana Machi 31, 2018
kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, ambapo
amesisitiza kuwa ni muhimu wasaidizi wa Mufti wakasimamia suala hilo.
Waziri Mkuu amesema amani ni miongoni mwa
neema kubwa sana kwa binadamu na ndio maana wote wanamtambua Mwenyezi
Mungu, hivyo wasiruhusu mtu au kikundi chochote kujaribu kuchafua na
kuharibu amani iliyopo nchini.
“Dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu
ya kila siku ndio maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote
kutokana na mchango wake mkubwa katika amani ya nchi yetu. Niwaombe
viongozi wangu popote mlipo muilinde amani yetu”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewasisitiza viongozi Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
wahakikishe kuwa wanaedelea kuwaunganisha waislamu bila ya kujali
makabila yao, rangi zao au madhehebu yao.
Waziri Mkuu amesema Mufti wa Tanzania Sheikh
Aboubakar bin Zubeiry ambaye ndiye kiongozi wa Waislamu nchini mara
zote amekuwa akisisitiza jambo hilo na kuwataka waislamu popote walipo
watambue kuwa hicho ni chombo chao.
“Ni muhimu sana kwa ninyi wasaidizi wa Mufti
mlio kusanyika hapa muhakikishe mnalisimamia hili katika maeneo yenu.
Katika hili napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko pamoja
Mheshimiwa Mufti kutekeleza nia hiyo njema.”
Amesema ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ni kuwa
Serikali anayoiongoza ipo tayari kusikiliza maoni, ushauri na
mapendekezo yeyote kutoka kwa viongozi wa dini.
Ameongeza kuwa yeye si mtaalamu sana kama
walivyo Masheikh hao lakini anakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu ndani ya
Qur’ani sura Al Imran aya ya 103 yanayosema “ Shikamaneni na kamba ya
Mwenyezi Mungu nyote na wala msifarakane”
Mkutano huo umehudhuriwa na Sheikh Mkuu wa
Mufti wa Tanzania Sheikh Zubeir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Masheikh na viongozi wa BAKWATA wa mikoa na
wilaya zote Tanzania.
Comments
Post a Comment