Mbunge
wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko
amewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Lyobahika , Kata ya Uyovu Wilayani Bukombe
kuwa wote waliohusika na tukio la ujambazi lililotokea hapo Aprili 11,
2018 na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba watakamatwa.
Biteko
alibainisha hayo Aprili 12,
2018 alipofika kutoa pole kwa wananchi wa
eneo kulikotokea tukio la ujambazi lililosababisha uharibifu mkubwa wa Mali za Emanuel Samwel Sayi maarufu Ndokeji na kuporwa
kiasi cha Shilingi Milioni Arobaini na vifaa vingine ikiweno simu za
mkononi.
Akizungumzia tukio hilo, Mtendaji wa
Kata Bartazari alisema tukio hilo lilitokea majira ya Saa Sita
na Nusu usiku ambapo watu wasiofahamika walivamia eneo hilo wakiwa na
silaha za moto ambapo walichoronga na kuweka kitu chenye mlipuko na kubomoa ukuta wa nyuma wa duka hilo na kufanikiwa kupora.
Biteko
aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali inafuatilia suala hilo kwani
ni jukumu lake kuhakikisha usalama kwa wananchi wake.
Alimuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Runzewe kuhakikisha uchunguzi unakamilika mapema ili kuwabaini wahusika wote wa tukio hilo.
"Serikali itahakikisha wale wote waliouhusika na tukio hili wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake,"alisisitiza Biteko.
Aidha Biteko alisema taarifa alizopata
ni kwamba matukio ya uhalifu yameongezeka Jimboni humo na aliiagiza
Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha upelelezi unafanyika ili
kukomesha matukio mbalimbali ya kihalifu.
Aliwataka wananchi jimboni humo kuendeleza ulinzi shirikishi na kuwabaini na
kuwataja wananchi wanaotishia usalama kwenye maeneo mbalimbali.
"Haya
matukio kuna wananchi hapa lazima wanahusika ambao wanatoa taarifa kwa
wahalifu kuhusiana na hali ya hapa. Wananchi msiogope kuwataja
mnaowashakia ili hatua zichukuliwe," alisema.
Mbunge
na Naibu Waziri huyo alifika Jimboni humo kwa ajili ya kutoa pole kwa wahanga hao ikiwemo wazazi wake ambao pia walivamiwa nyumbani kwao Kijiji cha Imuhozyo Kata ya Bulangwa.
Comments
Post a Comment